Mofimu

Mofimu ni sehemu ndogo zaidi ya neno inayowakilisha maana ya neno hilo. Mofimu inaweza kuwa silabi moja au zaidi.
Kuna aina mbili za mofimu:

  1. Mofimu huru
  2. Mofimu Tegemezi

1. Mofimu huru


Mofimu huru ni silabi moja au zaidi yenye maana kamili ya neno na inaweza kujisimamia yenyewe bila msaada wa viambishi au silabi nyingine. Aghalabu mofimu huru huwa nomino, vivumishi au vielezi visivyochukua viambishi vya ngeli.
Kwa mfano:daktari, ndoa, nyumba, Miranda

2. Mofimu Tegemezi


Mofimu tegemezi ni mofimu ambazo huhitaji viambishi au mofimu nyingine tegemezi ili kuleta maana iliyokusudiwa. Mofimu hizi hujumuisha hasa mzizi wa neno (au shina la kitenzi), vivumishi, nomino au vielezi ambavyo vinahitaji viambishi viwakilishi vya ngeli ili kutoa maana iliyokusudiwa.
Shina la kitenzi au mzizi wa neno au kiini cha kitendo ni sehemu ndogo zaidi inayosimamia kitenzi chenyewe bila mnyambuliko, nyakati au viambishi vinginevyo. Viambishi ni mofimu tegemezi ya silabi moja inayowakilisha dhana fulani kama vile hali, ngeli, nafsi, wakati na kadhalika.
k.m:
mtangazaji => m-tangaz-a-ji
{
m => mofimu ya ngeli ya M-WA kwa umoja
tangaz => mzizi wa neno, kiini cha kitendo cha kutangaza
a => kiishio cha kitenzi
ji => inaonyesha kazi au mazoea
}

wametusumbua => wa-me-tu-sumbu-a
{
wa => kiambishi kiwakilishi cha nafsi ya tatu wingi
me => kiambishi cha wakati timilifu
tu => kiambishi kiwakilishi cha nafsi ya kwanza wingi - kitendewa/mtendwa
sumbu => shina la kitendo cha kusumbua
a => kiishio
}

wakulima => wa-ku-lim-a
{
wa => kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya A-WA wingi
ku => kiambishi cha KU ya kitenzi jina
lim => mzizi wa kitendo cha kulima
a => kiishio
}