Tungo Fupi

Tungo Fupi ni kipera cha Fasihi Simulizi kinachojumulisha sanaa simulizi zinazoundwa kwa maneno machache; sentensi moja au mbili hivi. Tungo Fupi nyingi huwa na sehemu mbili na aghalabu huhitaji kujibizana ambapo mtu mmoja hutoa pendekezo au swali; halafu mtu mwengine hutoa jawabu - k.m vitendawili na mafumbo. Baadhi ya tungo fupi husemwa na mtu mmoja tu kama vile methali.

Aghalabu vipera vyote vya tungo fupi hutumiwa katika kazi nyingine za fasihi ( na lugha kwa ujumla ) kama mapambo ya lugha.

Vipera vya Tungo Fupi

  1. Methali
    Methali ni tungo fupi za sentensi moja ambazo hutoa funzo fulani kwa njia ya mafumbo. Methali huwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza hutoa hoja nayo sehemu ya pili hutoa suluhisho. Methali hutumika kwa minajili ya kutoa funzo kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Methali nyingine huhitaji hekima ili kujua maana yake.
  2. Vitendawili
    Vitendawili ni tungo fupi ambazo huwa na swali fupi na jibu kwa makusudi ya kupima ufahamu wa hadhira kuhusu mazingira yake. Anayetoa kitendawili huulizia swali lake kwa kutoa maelezo mafupi yanayorejelea umbo la kitu hicho, sauti, harufu au kukifananisha na kitu kingine. Anayejibu huhitajika kufikiria haraka na kutoa jawabu ambalo huwa la neno moja au maneno mawili hivi. Vitendawili huwa na mianzo maalum kulingana na jamii yake.
  3. Mafumbo
    Mafumbo hutumika kuupima uwezo wa mtu kufikira na kufumbua swali ambalo huwa na maelezo marefu. Majibu ya mafumbo huhitaji maelezo na aghalabu hukusudia kujua jinsi mtu anavyoweza kutatua tatizo fulani ambalo linahitaji kufikiria sana.
  4. Vitanza Ndimi
    Vitanza ndimi huwa ni sentensi zinazotumia maneno yanayomkanganya msomaji katika matamshi. Vitanza ndimi huhitaji kutamkwa haraka haraka na kurudiwa rudiwa mara kadhaa kwa kusudi la kukuza uwezo wa kutamka.
  5. Vichezea Maneno
    Ni maneno yanayokaribiana kimatamshi au kimaana hutumika katika sentensi moja kama njia ya kuonyesha ukwasi wa lugha au kuburudisha. Pia hutumika kama vitanza ndimi.
  6. Misimu
    Misimu ni maneno ambayo huzuka miongoni mwa kundi fulani katika jamii na hueleweka tu miongoni mwa watu katika kundi hilo. Misimu hukua na kutoweka baada ya muda.
  7. Lakabu
    Lakabu ni majina yanayobandikwa watu kutokana na sifa zao, maumbile, hulka au mambo yanayowahusu. Lakabu pia ni mbinu ya sanaa.
  8. Semi (Nahau na Misemo)
    Semi ni mafungu ya maneno ambayo hutumika kuleta maana tofauti na maana halisi ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha maneno makali kwa kutumia maneno mengine. Aidha semi zinaweza kutumika tu kwa minajili ya kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi: Nahau na misemo