Matumizi ya Viungo Mbalimbali

Katika mada hii, tunaangazia viambishimaneno ya silabi moja yanayotumika sana kwa Kiswahili kuwakilisha dhana mbalimbali.
Kwa sasa tumekuandalia matumizi ya:


KI | KU | KWA | NI | NA | KA | PO | JI




Matumizi ya KI

  1. Kiambishi Kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI

    1. Kiatu kilichochomeka kilikuwa kimeharibika.
    2. Kisiwa hiki kilichohamwa hakikaliki.

  2. KI ya Masharti

    1. Ukitaka kufua dafu, lazima utie bidii.
    2. Ukicheka sana utavunjika mbavu.
    3. Nitazichukua zikianguka.

  3. KI ya Mfanano - Kulinganisha(Vivumishi na vielezi vya Ki-Mfanano)

    1. Watu wa Mizukani wanaabudu kishetani.
    2. Amevalia mavazi ya kifalme.
    3. Msichana huyo huongea kimalaika.

  4. KI ya Udogo

    1. Kijiji chao ni mahame.
    2. Kitabu kile kimejifunga.

  5. Kuonyesha kinatendeka wakati mmoja na kitendo kingine

    1. Kesha alipobisha, Mganga Kuzimu alikuwa akila nzi.
    2. Tulimkuta akichoma mhindi. Mama alicheka mtoto akilia.

  6. Kukanusha kauli ya kutendeka

    1. Wasichana warembo huoleka => Wasichana warembo hawaoleki.
    2. Sauti nzuri zinasikika => Sauti nzuri hazisikiki.

  7. Kiambishi Kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI

    1. Ikiona vyalea vyaundwa.
    2. Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.

  8. Kutangulia majina ya lugha mbalimbali

    1. Ali Kiba huimba kwa Kiswahili.
    2. Kiingereza ndiyo lugha ya Wazungu kutoka Uingereza.



Matumizi ya KU

  1. Kiambishi Kiwakilishi cha Ngeli ya mahali KU-KU

    1. Shuleni hakuna usalama.
    2. Huku kumekauka sana.

  2. Kuanzisha vitenzi vya silabi moja au hali kamilifu ya kitendo.

    1. Ninataka kula.
    2. Walikuja jana asubuhi.

  3. Kuanzisha nomino za kitenzi jina.

    1. Kuchekacheka kwake kulimsaliti.
    2. Kuimba kwenu hakunipendezi.

  4. Kuanzisha vitenzi katika hali ya kawaida au kitenzi cha pili katika vitenzi sambamba.

    1. Kisu hutumika kukatia vitu.
    2. Wamekwenda kupiga ngoma.

  5. Kiambishi cha Kukanusha Wakati Uliopita

    1. Maji yako hayakumwagika.
    2. Sikuingia kwenye chumba kile.

  6. Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa/mtendewa nafsi ya pili.

    1. Watoto watakuchekelea ukivalia viatu vya manjano.
    2. Sijakueleza jinsi nilivyopambana na simba mwenye njaa.



Matumizi ya KWA

  1. Kuonyesha umiliki wa mahali

    1. Sheila amekwenda kwa Bi Mashaka.
    2. Kwa akina Kawia ni mbali kutoka Vikwazoni.

  2. Kutolea sababu au nia na Kuulizia Sababu

    1. Umeadhibiwa kwa kukosa nidhamu.
    2. Kali amelala mapema kwa kuwa anaenda shule mapema kesho.
    3. Ni kwa nini binadamu hawamheshimu Mungu

  3. Kuonyesha sehemu ya kitu kizima (akisami)

    1. Katika mtihani walioufanya, Jabu alipata kumi na tatu kwa ishirini (13/20).
    2. Sehemu ya nne kwa tano (4/5) ya ndizi hizi imeoza.

  4. Kulinganisha

    1. Timu yao ilishindwa mabao mawili kwa sufuri.
    2. Rita na Anita wanafanana kama shilingi kwa ya pili

  5. Kuonyesha muda uliochukuliwa na kitendo

    1. Tulimsubiri kwa masaa mawili kisha tukaondoka.
    2. Yeye huoga kwa muda mfupi sana.

  6. Kuelezea Ala au kitumizi

    1. Alikuwa akilima kwa jembe kuukuu.
    2. Walikuja kwa basi.

  7. Kuelezea Mbinu, Jinsi au Namna

    1. Kaombi alipata pesa kwa kuandaa harambee.
    2. Mgonjwa aliongea kwa uchungu mwingi sana

  8. Hutumika katika misemo

    1. Kesha na Nuru waliketi sako kwa bako.
    2. Mshindi alibebwa juu kwa juu



Matumizi ya NI

  1. Kiambishi kiwakilishi cha Nafsi ya Kwanza umoja

    1. Nitakapokasirika watanitambua.
    2. Nitayainua macho yangu nitazame milima.

  2. Kiunganishi cha wakati uliopo kuonyesha hali au sifa ya kitu.

    1. Katosha ni msichana mpole sana.
    2. Tegemeo letu ni kufika Mbinguni.

  3. Kiambishi kiwakilishi cha kielezi cha mahali

    1. Nyuki wamefukuza wavulana uwanjani.
    2. Shimoni humu hamna nuru.

  4. Kukanusha kauli ya kutendana, kutendeana

    1. Maji na mafuta hayatoshani uzani.
    2. Giza na nuru hazishirikiani.

  5. Kiishio katika hali ya kuagiza, kuamuru au kuhimiza nafsi ya pili wingi

    1. Wahubirini watu wote.
    2. Ondokeni enyi msioijua njia.
    3. Pokeeni baraka tele.

  6. Kukanusha kauli ya kutendeka

    1. Wasichana warembo huoleka => Wasichana warembo hawaoleki.
    2. Sauti nzuri zinasikika => Sauti nzuri hazisikiki.

  7. Kiambishi kiwakilishi cha vivumishi viulizi nini na kwa nini

    1. Pilipili usiyoila ya kuwashiani?
    2. Mama amenipigia simu mara sita leo, sijui ananitakiani.



Matumizi ya KA

  1. Kiambishi kiwakilishi cha Wakati Usiodhihirika

    1. Mama akamtuma mwanawe aende kuchota maji.
    2. Nikamwuliza anionyeshe sanduku lake.

  2. Katika vitenzi sambamba - kitendo kimoja kinapofanyika baada ya kingine

    1. Alikula akashiba kisha akalala.
    2. Tulifika nyumbani, baba akatuuliza tumewaacha wapi fahali.

  3. Kuagiza au Kuamuru

    1. 'Kalaleni!' Mama akawaamuru watoto.
    2. Kamwambie asirudi hapa tena.

  4. Kiishio cha kauli ya kutendeka

    1. Kijana mtundu alipigwa akapigika.
    2. Tulijaribu kufungua mlango lakini haukufunguka.



Matumizi ya NA

  1. Kiunganishi (cha Kujumuisha)

    1. Kikombe na bakuli ni vyombo vya jikoni.
    2. Jogoo alikatwa kichwa na kuchinjwa.

  2. Kiambishi kiwakilishi cha wakati uliopo

    1. Ninapenda kusoma riwaya za Kiswahili.
    2. Ukuta unazidi kupasuka.

  3. Kuonyesha umilikaji

    1. Selena ana sauti tamu.
    2. Kitanda kina kunguni weusi.

  4. Kiishio cha kauli ya Kutendana na kutendeana

    1. Tuliwaona fahali wawili wakipigana.
    2. Mwalimu amepeana onyo la mwisho.



Matumizi ya PO

  1. PO ya Mahali

    1. Mahali alipoanguka paliacha kuota nyasi.
    2. Hapo ndipo tulipoketi. Jumapili ifikapo tutakwenda Kisetoni.

  2. PO ya Wakati

    1. Nilipomlilia aliisikia sauti ya dua langu.
    2. Kitumbua kilipikwa mayai yalipoletwa.
    3. Zitakaporudishwa tutazificha mbali.

  3. PO ya Hisia(Hasira)

    1. Umenikosea sana! Po! Utakiona cha mtema kuni.



Matumizi ya JI

  1. Kuunda nomino kutokana na kitenzi.

    1. sema => msemaji.
    2. kimbia => mkimbiaji

  2. Kuonyesha Ukubwa

    1. Jikapu lile lina jitunda kubwa.
    2. Jito lile limemeza watu wengi.

  3. Kuonyesha mtendaji anapokuwa mtendewa (kujitenda, kujitendea)

    1. Amejikwaa kidole cha kati.
    2. Kitabu kimejifungua chenyewe.