Hii ni lugha inayotumiwa na watu katika familia. Wanaohusika sana katika mazungumzo ya nyumbani ni mama, baba, watoto, majirani na watu wa ukoo. Maswala yanayorejelewa sana ni yale yanayoiathiri jamii/boma hilo.
Sifa za Sajili ya Nyumbani
Sifa za sajili ya nyumbani hubadilika kulingana na mada inayorejelewa, wanaozungumza na hali katika boma.
Mfano wa Sajili ya Nyumbani
Baba: | Mama Kadara! Huyo mtoto wako amekuja? |
Mama: | Kadara ni mtoto wetu; mimi na wewe. |
Baba: | Hapana! Mimi sizai malaya. Huyo ni wako. Hata Bahati ni wako! Hakika wote sita ni wako… |
Mama: | Mume wangu unanifanya nikasirike bure tu. Mbona umeanza mafarakano tena. |
Baba: | Mafarakano! Mafarakano! Ni mimi niliyekwambia uzae wasichana sita… |
Mama: | Lakini sikuzaa pekee. Tulizaa na wewe, mume wangu…. |
Baba: | Hapana! Uliniona na mimba? Uliniona na maumivu ya uzazi? Umeniona nikinyonyesha mtoto? Mwanamke kuwa na adabu. Nitakurudisha kwa wazazi wakufunze heshima. Na nitaoa sioni tukikaa pamoja. |
Mama: | (baada ya kimya) Niambie ulichotaka kuniambia kuhusu Kadara (akijipangusa machozi kwa kitambaa) unajua mume wangu, nakuheshimu. Yangalikuwa mapenzi yangu tungepata wavulana pia. Lakini haya ni mapenzi ya Mungu. |
Baba: | Kadara akija umpe kuku apeleke vileoni kwa Mzee Magoti. Nina deni lake kubwa baada ya kunywa tembo siku kadhaa bila kulipa. (akicheka) Hakika hata anastahili mbuzi. |
Mama: | Hatuwezi kulipia pombe kwa mbuzi wala kuku. Kuku waliobaki hapa ni wangu na wa watoto wangu. Kuku wako uliwauza. |
Baba: | Kelele za chura hazimkatazi ng'ombe kunywa maji. Endelea kupayuka kama wanawake wengine wa kijijini. Nikirudi nikute chakula na maji moto tayari. |
Mama: | (akinuna) Haya nimesikia. |