Bahari za Ushairi

Bahari za ushairi ni nyingi sana. Shairi huainishwa katika bahari fulani kulingana na mtindo wake, umbo lake na matumizi ya lugha.

Mifano ya Bahari za Ushairi

  1. Utenzi - shairi ndefu lenye kipande kimoja katika kila mshororo.
  2. Mathnawi - ni shairi la vipande viwili (ukwapi na utao) katika kila mshororo.
    • Ewe mtunga silabi, na sauti ya kinubi,
    • Majukumu hatubebi, maadamu hatushibi,
    • Mateso kwa ajinabi, kwa mabwana na mabibi
    • Ukija hayatukabi, karibia karibia
  3. Ukawafi - ni shairi la vipande vitatu (ukwapi, utao na mwandamo) katika kila mshororo.
    • Nashindwa nikupe nini, nishukuru kwa malezi, mapenzi na riziki,
    • Ni pendo kiasi gani, lishindalo la mzazi, kweli mama hulipiki,
    • Ulinilinda tumboni, ukilemewa na kazi, ila moyo huvunjiki,
    • Kanilisha utotoni, mavazi pia malazi, ukitafuta kwa dhiki.
  4. Mavue - Shairi la vipande vinne (ukwapi, utao, mwandamo na ukingo) katika kila mshororo.
    • Sisi walipa ushuru, wajenga taifa, tena kwa bidii, twahangaishwa,
    • Tumenyimwa uhuru, tuna mbaya sifa, hatujivunii, tunapopotoshwa,
    • Kila tunapopazuru, damu na maafa, hatutulii, hali ya kutishwa
  5. Ukaraguni - shairi ambalo vina vyake vya kati na vya mwisho hubadilika kutoka ubetio mmoja hadi mwingine.
    • Vina Ubeti 1: ---ni, ---mi,
    • ubeti 2: ---ta, ---lo,
    • ubeti 3: ---po, ---wa,
  6. Ukara - shairi ambalo vina vya kipande kimoja havibadiliki kutoka ubeti mmoja hadi mwingine, lakini vina vya kipande kingine hubadilika. Kwa mfano, vina vya kati vinafanana kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho lakini vina vya kipande cha mwisho vinabadilika kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.
    • vina Ubeti 1: ---shi, ---ma,
    • ubeti 2: ---shi, ---ko,
    • ubeti 3: ---shi, ---le,
    • ubeti 4: ---shi, ---pa

      Mtiririko - shairi ambalo vina vyake vya mwisho na vya kati havibadiliki kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho. kwa mfano vina vikiwa ( ---ni, ---ka) kutoka ubeti wa kwanza hadi wa mwisho.
  7. Mkufu/pindu - Shairi ambalo neno la mwisho au kifungu cha mwisho cha maneno katika ubeti mmoja, hutangulia katika ubeti unaofuatia.
    • Hakika tumeteleza, na njia tumepoteza,
    • Nani wa kutuongoza, aliyepewa uweza,
    • Filimbi akipuliza, tusiyeweza kupuuza,
    • Bali twaisikiliza, bila ya kuzungumza,


    • Bila ya kuzungumza, wala mwendo kulegeza,
    • Tumwandame ja mwangaza, kututoa palipo giza,
    • Penye dhiki ya kuliza, bila sauti kupaza
    • Pengo hili kulijaza, ni nani anayeweza,
  8. Kikwamba - Neno moja au kifungu cha maneno hurudiwarudiwa kutanguliza mishororo au ubeti katika shairi.
    • Jiwe hili lala nini, ila moshi na majani,
    • Jiwe linalala lini, litokapo vileoni,
    • Jiwe hili halineni, lina macho halioni,
    • Jiwe na tulibebeni, tulitupe mitaroni
  9. Kikai - Shairi lenye kipande kimoja kifupi (chenye mizani chache kuliko kingine) Mfano (8,4)
    • Nani binadamu yule, adumuye,
    • Anayeishi milele, maishaye
    • Jenezani asilale, aluliye,
    • Kaburi liko mbele, sikimbiye.
  10. Msuko - Shairi ambalo kibwagizo/mshororo wa mwisho ni mfupi kuliko mishororo mingineyo. K.v (8,8) (8,8) (8,8) (8)
    • Hawajazawa warembo, usidhani umefika,
    • Ukisifiwa mapambo, jinsi ulivyoumbika,
    • Akipata jipya umbo, 'tabaki kihangaika,
    • Usidhani umefika.
  11. Mandhuma - shairi ambalo kipande kimoja hutoa hoja, wazo ama swali, huku cha pili kikitoa jibu/suluhisho.
  12. Malumbano - Mashairi mawili ambapo mshairi mmoja hutunga shairi akijibu au kupinga utunzi wa mshairi mwengine.
  13. Ngonjera - Shairi lenye wahusika wawili wanaojibizana. K.m. Ubeti wa kwanza, mwalimu, na wa pili, mwanafunzi.
  14. Sakarani - Shairi lenye bahari zaidi ya moja.
  15. Sabilia - Shairi lisilokuwa na kibwagizo. Kituo (mshororo wa mwisho) hubadilika kutoka ubeti hadi ubeti.
  16. Shairi huru - shairi lisilozingatia sheria za ushairi
  17. Shairi guni - shairi lenye makosa ya arudhi za shairi