Sajili ya Nyumbani

Hii ni lugha inayotumiwa na watu katika familia. Wanaohusika sana katika mazungumzo ya nyumbani ni mama, baba, watoto, majirani na watu wa ukoo. Maswala yanayorejelewa sana ni yale yanayoiathiri jamii/boma hilo.

Sifa za Sajili ya Nyumbani

Sifa za sajili ya nyumbani hubadilika kulingana na mada inayorejelewa, wanaozungumza na hali katika boma.

Mfano wa Sajili ya Nyumbani

Baba: Mama Kadara! Huyo mtoto wako amekuja?
Mama: Kadara ni mtoto wetu; mimi na wewe.
Baba: Hapana! Mimi sizai malaya. Huyo ni wako. Hata Bahati ni wako! Hakika wote sita ni wako…
Mama: Mume wangu unanifanya nikasirike bure tu. Mbona umeanza mafarakano tena.
Baba: Mafarakano! Mafarakano! Ni mimi niliyekwambia uzae wasichana sita…
Mama: Lakini sikuzaa pekee. Tulizaa na wewe, mume wangu….
Baba: Hapana! Uliniona na mimba? Uliniona na maumivu ya uzazi? Umeniona nikinyonyesha mtoto? Mwanamke kuwa na adabu. Nitakurudisha kwa wazazi wakufunze heshima. Na nitaoa sioni tukikaa pamoja.
Mama: (baada ya kimya) Niambie ulichotaka kuniambia kuhusu Kadara (akijipangusa machozi kwa kitambaa) unajua mume wangu, nakuheshimu. Yangalikuwa mapenzi yangu tungepata wavulana pia. Lakini haya ni mapenzi ya Mungu.
Baba: Kadara akija umpe kuku apeleke vileoni kwa Mzee Magoti. Nina deni lake kubwa baada ya kunywa tembo siku kadhaa bila kulipa. (akicheka) Hakika hata anastahili mbuzi.
Mama: Hatuwezi kulipia pombe kwa mbuzi wala kuku. Kuku waliobaki hapa ni wangu na wa watoto wangu. Kuku wako uliwauza.
Baba: Kelele za chura hazimkatazi ng'ombe kunywa maji. Endelea kupayuka kama wanawake wengine wa kijijini. Nikirudi nikute chakula na maji moto tayari.
Mama: (akinuna) Haya nimesikia.