Viwakilishi (W)

Viwakilishi vya Nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.

Aina za Viwakilishi

Viwakilishi vya Nafsi

Viwakilishi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi.

k.m: mimi, wewe, yeye, sisi, nyinyi, wao
NAFSI UMOJA WINGI
Nafsi ya Kwanza Mimi Sisi
Nafsi ya Pili Wewe Ninyi/Nyinyi
Nafsi ya Tatu Yeye Wao
  • Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa.
  • Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria

Viwakilishi Viashiria

Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.

k.m: huyu, yule, hapa, n.k
  • Hiki hakina maandishi yoyote.
  • Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi
  • Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.

Viwakilishi Visisitizi

Husisitiza nomino inayowakilishwa kwa kurudiarudia kiashiria chake.

k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu,
  • Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana
  • Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena.

Viwakilishi vya Sifa

Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.

k.m: '-eupe, -zuri, -tamu, -embamba, -rembo, safi'
  • Vyekundu vimehamisha
  • Warembo wamewasili.
  • Kitamu kitaliwa kwanza.

Viwakilishi vya Idadi

Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.

a) Idadi Kamili- hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.

k.m: 'saba, mmoja, ishirini'
  • Wawili wamepigwa risasi polisi leo jioni.
  • Alimpatia mtoto wake hamsini kununua chakula

b) Idadi Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili

k.m: 'chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani'
  • Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.
  • Kadhaa zimeripotiwa kupotea.

Viwakilishi Viulizi

Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.

Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli

k.m: ' -ngapi?, -pi?'
  • Vingapi vinahitajika? - kuulizia idadi
  • Zipi zimepotea?

Kunavyo viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.

k.m: 'wapi?, gani?, nini?, vipi?'
  • Gani imefunga bao hilo?
  • Wapi hapana majimaji?
  • Yule mvulana alikupatia nini?
  • Uliongea naye vipi? - kuulizia namna

Viwakilishi Vimilikishi

Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.

k.m: '-angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao '
  • Kwetu hakuna stima.
  • Lake limekucha.
  • Zao zimeharibika tena

Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)

Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino

k.m: 'ambaye, ambao, ambalo, ambacho, huyo, yule'
  • Ambalo lilipotea limepatikana.
  • Ambaye hana mwana, aeleke jiwe

Viwakilishi Vya A-Unganifu

Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine

k.m: 'cha, la, kwa, za, ya'
  • Cha mlevi huliwa na mgema
  • Za watoto zitahifadhiwa.