Hotuba

Insha ya hotuba ni insha ambayo hutoa maneno halisi ya mzungumzaji/hatibu/kiongozi anapozungumzia hadhira, kuhusu jambo fulani. Insha ya hotuba huandikwa katika hali ya usemi halisi na mwandishi hatakiwi kuweka alama za kunukuu anapoanza insha yake.

Hotuba inaweza kutolewa na kiongozi wa kisiasa, utawala, kidini, kikundi, shirika fulani, daktari, n.k. Hadhira katika hotuba husheheni wageni waalikwa, wanachama, wafuasi, wananchi, n.k ambao wanahusishwa katika mada inayorejelewa katika hotuba hiyo. Mengi ya maswala yanayojitokeza katika insha za hotuba ni maswala ibuka katika jamii k.v upangaji wa uzazi, usalama, n.k

Muundo wa Hotuba

  1. Anwani

    Anwani, mada au kichwa cha hotuba huchukua herejelea hatibu pamoja na mada ya hotuba. Pia mada inaweza kutaja hadhira.

    • Hotuba ya Waziri wa Afya kuhusu madhara ya ukimwi kwa wananchi.
    • Hotuba ya Mwalimu Mkuu kwa Wazazi
  2. Utangulizi

    • Anza hotuba yako kwa kuwatambua waliohudhuria mkutano (hadhira).
    • Wataje kwa majina/vyeo vyao kuanzia yule wa cheo cha juu hadi wa chini, mabibi na mabwana. Kumbuka kwamba hauhitajiki kuwasalimia. Kuwatambua kwa majina pekee kunatosha.
    • Jitambulishe kwa hadhira yako hasa ikiwa unazungumzia hadhira isiyokujua au wageni.
    • Tanguliza mada yako. Kwa mfano:
      Waziri wa Kilimo, Mkuu wa Wilaya, Chifu wa Kisioni, wanachama wa kikundi hiki cha Rotuba Bora, mabibi na mabwana. Ni matumaini yangu kwamba nyote mu buheri wa afya. Mimi ni mwakilishi wa Kikundi cha Mshipi wa Kijani Kibichi na jioni ya leo kuna jambo muhimu ambalo ningependa sote tulifahamu ili kuboresha mazingira yetu kwa ...
  3. Mwili

    • Hakikisha kuna mtiririko wa hoja kuanzia mwanzo hadi mwisho
    • Ujumbe wako wote unapaswa kuwa katika usemi halisia wala si wa taarifa.
  4. Tamati

    • Hakikisha kwamba mwisho wa hotuba yako unatambulika.
    • Unaweza kumaliza kwa shukurani

Mfano ya Insha za Hotuba:

  1. Wewe ni chifu katika kijiji cha Kikanyageni. Andika hotuba utakayotoa kwa vijana kuhusu hatua za serikali kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.
  2. Umealikwa kuwahutubia wanafunzi wa shule ya msingi uliyosomea kuhusu umuhimu wa elimu ya wasichana. Andika hotuba utakayotoa.
  3. Wewe ni daktari. Andika hotuba utakayotoa kuwahimiza wanawake wakubali kutumia mbinu za kupanga uzazi.
  4. Umeteuliwa na afisa katika idara ya utalii kuhutubia watalii kuhusu changamoto za kiusalama zinazolikabili bara hili na upendekeze mbinu za kuzitatua.