Vielezi (E)

Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi au vielezi vingine.

Aina za Vielezi

Vielezi vya Mahali

Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.

k.m: nyumbani, kazini, shuleni
  • Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
  • Msipitie sokoni mkienda kanisani.

Vielezi vya Wakati

Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika

k.m: jioni, jana, asubuhi, saa saba, mwaka juzi
  • Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
  • Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
  • Kisaka na Musa watakutana kesho

Vielezi vya Idadi

Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi

a) Idadi Kamili

Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika.

k.m: mara mbili, siku mbili kwa juma, mara kumi
  • Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
  • Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi

b) Idadi Isiyodhihirika

Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili

k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
  • Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
  • Yeye hunipigia simu mara kwa mara

VIelezi Vya Namna

Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:

a) Vielezi vya Namna Halisi

Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine).

k.m: vizuri, ovyo, haraka
  • Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
  • Mama alipika chakula upesi
  • Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela

b) Vielezi vya Namna Hali

Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo

k.m: kwa furaha, kwa makini,
  • Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
  • Mtoto alilia kwa maumivu mengi

c) Vielezi vya Namna Kitumizi/Ala

Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani

k.m: kwa kisu, kwa jembe, kwa meno, kwa moto, kwa maji
  • Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
  • Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa

d) Vielezi Vikariri

Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo.

k.m: haraka haraka, ovyo ovyo, juu juu
  • Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
  • Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo

e) Vielezi vya Ki-Mfanano

Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha.

k.m: kitoto, kiungwana,
  • Babake huongea kiungwana.
  • Harida hutembea kijeshi

f) Vielezi Viigizi

Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti

k.m: tuli, chubwi, tifu, chururu
  • Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
  • Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi

g) Vielezi vya Vielezi

Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo

k.m: sana, kabisa, hasa, mno
  • Mamake Kajino alitembea polepole sana.
  • Chungu kilivunjika vibaya kabisa

h) Vielezi vya Vivumishi

Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi

k.m: sana, kabisa, hasa, mno
  • Yeye ni mrefu sana
  • Mtoto wake ana tabia nzuri mno