Msamiati wa Majina ya Ukoo

Haya ni majina ya heshima yanayotumiwa na watu mbalimbali katika familia kulingana na uhusiano wao. Pia huitwa msamiati wa nasaba/jamaa/jamii

Mifano

Familia Ndogo

Hii ni familia ya karibu, familia ya nyuklia (nuclear family) ambayo uhusisha tu wazazi na watoto wao.

  1. baba:
    ni mzazi wa kiume.
  2. mama:
    mama ni mzazi wa kike.
  3. mwana:
    mtoto wako
  4. mzazi:
    mtu aliyekuzaa
  5. ndugu:
    mtoto wa mzazi/wazazi wako. Mara nyingi 'ndugu' hutumika kurejelea watoto waliozaliwa baada yako, au watoto wa kiume waliozaliwa na wazazi wako.
  6. kaka:
    mvulana aliyezaliwa na mzazi/wazazi wako. Aghalabu kaka hurejelea mvulana aliyekutangulia kuzaliwa.
  7. dada:
    msichana aliyezaliwa na mzazi/wazazi wako. Aghalabu dada hutumika kurejelea wasichana waliokutangulia kuzaliwa.
  8. bin:
    mtoto wa kiume
  9. binti:
    mtoto wa kike.
  10. kifungua mimba:
    mtoto wa kwanza kuzaliwa
  11. kitinda mimba:
    mtoto wa mwisho kuzaliwa
  12. mapacha:
    watoto wawili waliozaliwa siku moja na mama mmoja
  13. mke:
    mwanamke mliyefunga ndoa pamoja kuanzisha familia.
  14. mume:
    mwanamume mliyefunga ndoa pamoja ili kuanzisha familia.
  15. baba wa kambo:
    mwanaume aliyeoa mamako, na ambaye si baba yako wa damu
  16. mama wa kambo:
    mwanamke aliyeolewa na babako, na ambaye si mama yako wa damu

Familia Kubwa

Familia Kubwa huhusisha familia ndogo pamoja na wazazi wa baba/mama, ndugu za baba na mama, pamoja na watoto wao. Kwa Kiingereza, familia hii huitwa Extended Family.

  1. babu:
    mzazi wa kiume wa mzazi wako. baba ya mama yako au baba yako.
  2. nyanya:
    mzazi wa kike wa mzazi wako. mama aliyemzaaa mamako au babako.
  3. mjukuu:
    mtoto wa mtoto wako
  4. mjomba:
    mvulana aliyezaliwa na babu au nyanya yako. Aghalabu mjomba hutumika kurejelea ndugu wa kiume wa mama yako. Katika mfumo huo, mvulana aliyezaliwa kabla ya babako huitwa baba mkubwa naye yule aliyezaliwa baada ya babako huitwa baba mdogo
  5. shangazi:
    msichana aliyezaliwa pamoja na mzazi wako. Aghalabu shangazi hutumika kurejelea ndugu wa kike wa baba yako. Katika mfumo huo, msichana aliyezaliwa kabla ya mamako huitwa mama mkubwa naye msichana aliyezaliwa baada ya mamako huitwa mama mdogo
  6. mpwa:
    mtoto wa ndugu yako
  7. amu:
    ndugu wa mzazi wako.
  8. binamu:
    mtoto wa mjomba wako
  9. bintiamu:
    mtoto wa kike wa mjomba wako. binamu wa kike.
  10. shemeji:
    ndugu wa mkeo au mumeo. ndugu wa mke wa kakako, ndugu wa mume wa dadako. undugu unaotokana na ndoa.
  11. wifi:
    mke wa ndugu yako.
  12. mkwe:
    mzazi wa mke wako au mume wako.
  13. mkaza mjomba:
    mke wa mjomba wako
  14. mkaza mwana:
    mke wa mtoto wako
  15. bavyaa:
    baba mkwe. baba aliyemzaa mke wako au mume wako
  16. mavyaa:
    mama mkwe. mama aliyemzaa mke wako au mume wako

Nasaba - Vizazi

Huu ni mpangilio wa watu wa ukoo mmoja kulingana na vizazi mbalimbali. Orodha hii imepangwa kulingana na mpangilio wa mzazi > mtoto > n.k

  1. babu mkuu, nyanya mkuu:
    mzazi wa babu au nyanya yako
  2. babu, nyanya:
    mzazi wa baba yako au mama yako
  3. mzazi:
    mtu aliyekuzaa
  4. mwana:
    mtoto wako
  5. mjukuu:
    mtoto wa mtoto wako
  6. kitukuu:
    mtoto wa mjukuu.
  7. kinying'ina:
    mtoto wa kitukuu.
  8. kilembwe:
    mtoto wa kinying'ina.
  9. kilembwekeza:
    mtoto wa kilembwe.
  10. kitojo:
    mtoto wa kilembwekeza.