Vihisishi (I)

Vihisishi ni maneno yanayotumika kuonyesha hisia kama vile hasira, furaha, mshangao, kusifia, kushangilia n.k. Vihisishi hutambulishwa katika sentensi kwa kuambatanishwa na alama ya mshangao (!). Kihisishi kimoja kinaweza kutumika kutoa hisia tofauti kulingana na muktadha.

Mifano ya Vihisishi

Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya maneno yanayotumika kuonyesha hisia. Hata hivyo, maneno mengine yoyote yanaweza kutumika kama vihisishi, kulingana na mukhtadha. k.v Potelea mbali!

Kihisishi Mfano katika Sentensi Hisia
Lo! Lo! Maajabu ya Musa haya! mshangao
Salaale!, Masalaale! Salaale! Angalia watu wote hawa waliofika mahali hapa! mshangao
Kumbe! Nilidhani wewe ni rafiki yangu. Kumbe! mshangao
Po! Sijawahi kuona kijana mjeuri kama wewe. Po! hasira
Ng'o! Omba msamaha utakavyo, lakini unachoka bure. Ng'o! kiburi
Hata! Bwanake hakumwachia chochote! Hata! kusifia, kupuuza
Akh!, Aka! Mtoto mpumbavu huyu! Akh! hasira, kukashifu
Ah! Ah! Sikuyaamini macho yangu. mshangao
Ala! Ala! Umefika tayari! mshangao
Haha! Haha! Umenivunja mbavu, bwana! kicheko
Ehee!, Enhe! Enhe! Endelea, ninaipenda sana hadithi hiyo! kuitikia
Hmmm! Hmmm! Chakula kitamu hicho! kuitikia, kusifia
Ebo! Ebo! Tabia gani hiyo. kukashifu, hasira
Kefule! Kefule! Umenifedhehesha sana. hasira
Wee! Katamu alinegua kiuno na kucheza kwa madaha. Wee! Wavulana wakaduwaa. kusifia
La!, Hasha! La! Sitaki kusikiliza upuuzi wako tena. kukataa
Hoyeee! Wamama wote, hoyee! Hoyee! kushangilia
Huraa! Huraa! Tumeshinda. kushangilia