Sauti za Kiswahili

Sauti ni sehemu ndogo kabisa ya neno ambayo haiwezi kugawika zaidi. Sauti nyingi huwa ni herufi moja ya alfabeti kama vile (a, b, d) lakini kunazo sauti zinazoundwa kwa kuungunisha herufi mbili au zaidi (kama vile ng, nd, mb).

Alphabeti ya Kiswahili: a, b, ch, d, e, f, g, h, i, k, l, m, n, o, p, r, s, t, u, v, w, y, z

Kuna aina mbili za Sauti katika lugha ya Kiswahili:

  1. Irabu
  2. Konsonanti

Irabu (Vokali)

(a, e, i, o, u)

Irabu zinapotamkwa, hewa haizuiliwi katika ala za matamshi.

Jedwali lifuatalo litakuonyesha jinsi ya kubainisha vokali kulingana na sehemu ya ulimi inayoachilia hewa, na jinsi midomo inavyobadilika

Irabu Sehemu ya Ulimi Midomo
e,iMbele Midomo imetandazwa
a Katikati; ulimi huinuka na kutandaza Midomo imetandazwa
o,u Nyuma Midomo imevirigwa

Konsonanti

(b, ch, d, f, g, h, j, k, l, m, n, p, r, s, t, v,w, y, z)

Konsontanti zinapotamkwa, hewa huzuiliwa katika ala za matamshi ( ulimi na midomo). Kuna aina mbili kuu za sauti za konsonanti:

  1. Sauti Ghuna => konsonanti hizi zinapotamkwa, hewa hutikisa nyuzi za sauti
  2. Sauti Sighuna => konsonanti hizi zinapotamkwa, hewa haitikisi nyuzi za sauti

Jedwali lifuatalo litakuonyesha aina za konsonanti kulingana na mahali zinapotamkiwa na sauti (ghuna au sighuna)

MidomoMidomo + MenoMeno + Ulimi Ufizi Kaakaa + ufizi Kaakaa gumu Kaakaa Laini Koo Aina ya Sauti
Vipasuo pd td j kg sighuna ghuna
Vikwamizo / Vikwaruzo f v th dh sz sh khgh h sighuna ghuna
Kipasuo - kwamizo ch sighuna
Nazali / Ving'ong'o m n ny ng' ghuna
Kitambaza l ghuna
Kimadende r ghuna
Viyeyusho / Nusu Irabu y w ghuna

Vipasuo ( p,b,k,g,t,d )

Hutamkwa kwa kukutanisha ala za kutamkia ili kufungilia hewa na kisha kuiachilia ghafla

/p/ na /b/ hutamkwa kwa kukutanisha midomo katika meno:

/t/ na /d/ hutamkwa kwa kukutanisha ufizi na ncha ya ulimi

/k/ na /g/ hutamkwa kwa kukutanisha nyuma ya ulimi na kaakaa laini

Vikwamizo ( d f,v,dh,th, s,z,sh,h,gh)

Pia huitwa Vikwaruzo. Hutamkwa kwa kukutanisha ala za matamshi na kisha kuachilia hewa kupitia katika mwanya mwembamba

/f/ na /v/ hutamkwa kwa kukutanisha mdomo wa chini na wa juu na kuachilia hewa kidogo kupita

/s/ na /z/ hutamkwa kwa kukutanisha sehemu ya kati ya ulimi na kaakaa gumu

/dh/ na /th/ hutamkwa kwa kukutanisha ncha ya ulimi na meno ya juu

/gh/ na /kh/ hutamkwa kwa kukutanisha kaakaa laini na kilimi

/h/ hutamkwa kwa kukutanisha kilimi na koo na kuachilia hewa kwa nguvu

Kipasuo-kwamizo: ( ch )

Pia huitwa kituo-kwamizo. Hutamkwa kwa kukutanisha ulimi na ufizi, na kuachilia hewa

Ving'ong'o / Nazali ( m,n,ng',ny )

Hutamkwa kwa kukutanisha ala za matamshi na kuzuia hewa kupitia kinywani; hewa hupitia puani.

/m/ hutamkwa kwa kukutanisha mdomo wa juu na wa chini, ili kuzuia pumzi kupita kinywani

/n/ hutamkwa kwa kukutanisha ulimi na ufizi, ili hewa ipitie puani

/ny/ hutamkwa kwa kukutanisha ulimi na kaakaa gumu

/ng'/ hutamkwa kwa kukutanisha ulimi na kaakaa laini

Kitambaza ( l )

Hutamkwa kwa kukutanisha ncha ya ulimi na ufizi huku hewa ikipitia kwenye pande za ulimi bila kukwaruza ufizi

Kimadende ( r )

Hutamkwa kwa kupigapiga na kukwaruza ufizi haraka haraka kwa ncha ya ulimi.

Viyeyusho ( y,w )

Pia huitwa nusu-irabu. Hutamkwa kwa utaratibu kwa kuleta ala za matamshi karibu sana lakini kuachilia hewa bila kuikwaruza.

/w/ hutamkwa midomo ikiwa wazi

/y/ hutamkiwa kwenye kaakaa gumu

Ala za Kutamkia

Hizi ni sehemu za mwili zinazotumika wakati wa kutamkia maneno: '' Meno, Ulimi, Midomo, Pua, Chemba cha Pua, Ufizi, Kaakaa gumu, Kaakaa laini, Kimio , Chemba cha Kinywa, Ncha ya ulimi, Bapa la ulimi, Shina la Ulimi, Koromeo, Kidakatonge, Kongomeo, Nyuzi za Sauti, Koo, Njia ya Chakula ''