Fasihi
Fasihi ni sanaa ya lugha. Fasihi hutumia lugha kutoa sanaa mbalimbali katika jamii.
Tanzu za Fasihi
Kuna tanzu mbili kuu za fasihi, na kila utanzu una vipera vyake: Fasihi Simulizi na Fasihi Andishi:Fasihi Simulizi
- Hadithi (Ngano) - hekaya, mighani, visasili n.k
- Nyimbo - za jandoni, za ndoa, za kazi n.k
- Maigizo - michezo ya kuigiza, ngomezi n.k
- Tungo Fupi - methali, vitendawili n.k
Fasihi Andishi
- Hadithi Fupi - hadithi isiyokuwa ndefu iliyochapishwa katika mkusanyiko wa hadithi nyingine
- Riwaya - hadithi ndefu iliyochapishwa katika kitabu chake pekee
- Tamthilia - mchezo wa kuigiza uliowekwa kwa maandishi
- Ushairi* - mashairi yaliyoandikwa
Tanbihi:Ushairi ni kipera cha nyimbo lakini pia mashairi yanaweza kuwa chini ya Fasihi Andishi, ikiwa yamechapishwa.
Tofauti kati ya Fasihi Andishi na Fasihi Simulizi
FASIHI SIMULIZI | FASIHI ANDISHI | |
1. | Huwasilishwa kwa njia ya mdomo na/au matendo. | Huwasilishwa kwa njia ya maandishi |
2. | Ni mali ya jamii. | Kazi andishi ni mali ya mwandishi (na mchapishaji) |
3. | Msimulizi anaweza kubadilisha sehemu fulani | Kitabu kilichoandikwa hakiwezi kubadilishwa |
4. | Huhifadhiwa akilini | Huhifadhiwa vitabuni |
5. | Kazi simulizi hubadilika na wakati | Kazi andishi haibadiliki na wakati |
6. | Huhitaji msimulizi na hadhira yake wawe mahali pamoja wakati wa masimulizi | Msomaji anaweza kusoma kitabu cha hadithi peke yake, mahali popote, wakati wowote |
7. | Mtu yeyote anaweza kutunga na kusimulia | Ni lazima mwandishi na msomaji wawe na uwezo wa kusoma |
8. | Hutumia wahusika changamano (wanyama, watu, mazimwi n.k) | Hutumia wahusika wanadamu. |
Umuhimu wa Fasihi Katika Jamii
- Kuburudisha jamii. Takribani vipera vyote vya fasihi huwa na kusudi la kufurahisha, kutumbuiza na kusisimua hadhira.
- Kuelimisha. Fasihi hukusudia kuelimisha hadhira kuhusu jamii, mazingira n.k
- Kudumisha maadili katika jamii kwa kuelekeza, kuonya na kunasihi hadhira jinsi ya kufuata mwelekeo unaokubalika katika jamii.
- Kuunganisha jamii. Fasihi huleta pamoja watu katika jamii. Kwa mfano, katika nyimbo, miviga, vichekesho.
- Kukuza lugha. Aghalabu tungo zote za fasihi hutumia lugha. Isitoshe, fasihi hutumia mbinu nyingi za lugha. Wasimulizi na waandishi wa fasihi huhitaji kuwa na ukwasi wa lugha.
- Kuhifadhi mila, tamaduni na itikadi za jamii. Aghalabu kazi za fasihi (hasahasa Fasihi Simulizi) huambatanishwa na desturi mbalimbali za jamii husika.
- Kukuza uwezo wa kufikiri. Vipera vingi vya fasihi huwachochea hadhira kufikiri sana ili kupata suluhisho. k.m vitendawili, ngano za mtanziko n.k