Uchambuzi wa Mashairi

Yafuatayo ni mambo muhimu unayohitajika kuzingatia kila unapochambua shairi.

Muundo/Umbo la Ushairi

Katika umbo wa shairi, tunaangazia jinsi shairi lilivyoundwa kwa kuangazia mizani, vina, mishororo n.k Aidha, ni muhimu kutaja aina na bahari za shairi zinazohusiana na kila sifa uliyoitaja.

Uhuru wa Mshairi

Mshairi hafungwi na kanuni za kisarufi za lugha katika utunzi wa shairi. Anaweza kufanya makosa ya kisarufi kimakusudi ili shairi lizingatie umbo fulani. Zifuatazo ni njia mbalimbali ambazo mtunzi wa shairi anaweza kutumia kuonyesha uhuru wake.

 1. Inkisari - kupunguza idadi ya silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
  mfano: kubadilisha nimeona aliyenipenda kuwa meona alenipenda.
 2. Mazda - kuongeza silabi katika neno ili kusawazisha idadi ya mizani katika mshororo.
  mfano: afya ukijaliwa kuwa afiya ukijaliwa .
 3. Tabdila - kubadilisha silabi ya mwisho ili kustawazisha urari wa vina katika kipande bila kuathiri mizani.
  mfano: yahuzunisha dunia kuwa yahuzunisha duniya .
 4. Kuboronga Sarufi -ni mbinu ya kupangua mpangilio wa maneno ili kuleta urari wa vina au mdundo wa ushairi.
  mfano: siku hiyo ikifika kuwa ikifika hiyo siku .
 5. Utohozi - Kuswahilisha Maneno - Wakati mwingine mshairi anaweza kubadilisha neno la lugha nyingine litamkike kwa Kiswahili ili kudumisha mdundo wa kishairi na pia kupata neno mwafaka litakalotimiza arudhi za kiushairi.
  mfano: tukapata intaneti badala ya tukapata 'internet' ama mtandao wa tarakilishi.

Maudhui

Maudhui ni jumla ya ujumbe na mawazo mbalimbali yanayojitokeza katika shairi fulani. Haya ni mambo yanayotajwa katika hadithi na yanaweza kujumuisha mawazo zaidi ya moja. Maudhui husaidia kujenga dhamira ya shairi.

Dhamira

Dhamira ni lengo, dhumuni au nia ya mtunzi wa shairi. Mtunzi wa shairi anaweza kuwa na kusudi la kutuonya, kututahadharisha au kutunasihi kuhusiana na jambo fulani.

Mtindo wa Lugha

Mtindo wa lugha hurejelea namna mbalimbali ambazo mshairi anatumia mbinu za lugha. Mshairi anaweza kutumia mbinu za lugha. kama vile: Tanakali za Sauti, Istiara, Takriri, Semi n.k

Angalia: Mbinu za Lugha katika Fasihi