Tamathali za Usemi
Tamathali za Usemi ni matumizi ya maneno kwa namna fulani ili kuifanya lugha iwe ya kuvuitia na kuifanya kazi ya sanaa iwe ya kupendeza. Kuna aina mbili za tamathali za usemi:
- Mbinu au Fani za Lugha- Ni uteuzi wa maneno ili kuifanya lugha iwe ya kupendeza na kuvutia. Pia, Mapambo ya Lugha. Fani za Lugha zinaweza kutambulikana moja kwa moja bila kusoma kifungu kizima.
- Mbinu za Sanaa- Ni ubunifu wa kisanaa unaojitokeza baada ya kusoma au kusikiliza masimulizi. Angalau unahitaji kusoma sentensi kadhaa au hata hadithi nzima ili kutambua mbinu ya sanaa iliyotumika.
Mbinu za Lugha
- Tanakali za Sauti -Ni mbinu ya kutumia maneno yanayoiga sauti au hali fulani au namna kitendo kilivyofanyika. Milio.
- Tashbihi -Hii ni mbinu ya lugha inayolinganisha vitu au hali mbili tofauti kwa kutumia maneno ya kulinganisha; 'kama', 'mithili ya', 'sawa na', 'ja'. Tashbiha. Similes.
- Istiara -Ni mbinu ya kulinganisha vitu viwili moja kwa moja kwa kutumia kiungo 'ni' ama 'kuwa'. Istiari. Sitiari. Imagery
- Jazanda - Ni kulinganisha vitu viwili moja kwa moja bila kutumia viunganishi.
- Taashira - Ni matumizi ya lugha ya ishara kuwakilisha ujumbe fulani. Jina au kitu fulani kinatumika kumaanisha kitu kingine chenye uhusiano na kile kilichotumiwa. Symbolism
- Taswira - Ni matumizi ya lugha/maneno yanayojenga picha ya hali au jambo fulani kwa msomaji.
- Tashihisi - Hii ni mbinu ya kupatia kitu kisicho hai sifa za kiumbe mwenye uhai (sifa za kibinadamu). Uhuishaji. Personification.
- Chuku - Ni kutumia maneno yaliyotiliwa chumvi ili kusisitiza ujumbe fulani au kusifia kitu. Kutilia Chumvi. Hyperbole
- Takriri - Ni mbinu ya kurudiarudia neno moja au kifungu cha maneno ili kusisitiza ujumbe fulani. Repetition
- Tanakuzi- Tanakuzi ni mbinu ya kusisitiza ujumbe kwa kuambatanisha maneno ya kinyume au yanayokinzana. Ukinzani
- Majazi - Majazi ni pale tabia za wahusika zinapoambatana na majina yao halisi.
- Lakabu - Ni mbinu ya mhusika kupewa/kubadikwa jina na wahusika wengine ama yeye mwenyewe kujibandika jina linalooana na tabia/sifa zake.
- Semi - Ni fungu la maneno linapotumika kutoa maana nyingine, badala ya ile ya maneno yaliyotumika. Semi hutumika kuficha ukali wa maneno au kupamba lugha. Kuna aina mbili za semi:
- Nahau - huwa na vitenzi
- Misemo - haina vitenzi
- Methali - Methali ni misemo ya hekima yenye maana iliyofumbwa. Mhusika, mwandishi wa fasihi anaweza kutumia methali kupitisha ujumbe.
- Maswali ya Balagha - Tashititi au maswali ya balagha ni maswali yanayoulizwa na msimulizi au mhusika ambayo hayahitaji jibu. Mubalagha. (Rhetorical questions)
- Uzungumzi Nafsiya - Mhusika hujizungumzia, ama kwa kuongea au kuwaza, bila kukusudia kusikika na yeyote.
- Ritifaa - Mbinu ya kuzungumza na mtu aliyekufa (au asiyekuwepo) kana kwamba yuko pamoja nawe.
- Utohozi - Kutohoa ni mbinu ya kuswahilisha maneno ya lugha nyingine, yatamkike kama ya Kiswahili.
- Kuchanganya Ndimi - Kuweka maneno yasiyo ya Kiswahili katika sentensi ya Kiswahili.
- Kuhamisha Ndimi - Ni kuingiza sentensi ya lugha nyingine katika kifungu cha lugha ya Kiswahili. Kinyume na Kuchanganya ndimi (ambapo mwandishi huchanganya maneno katika sentensi moja, katika kuhamisha ndimi, sentensi kamilifu ya lugha nyingine hutumika miongoni mwa sentensi za Kiswahili sanifu.
Mbinu za Sanaa
- Kinaya - Kinaya ni mambo katika sanaa kuwa kinyume na matarajio ya hadhira. Irony
- Kejeli -Kejeli ni mbinu ya sanaa inayotumia maneno kudharau au kukemea kitendo au mtu fulani.
- Taharuki -Taharuki ni mbinu ya kusimulia au kuandika riwaya/hadithi kwa kufanya hadhira na/au wahusika wajawe na hamu ya kutaka kujua kitakachotokea baadaye; hamu ya kutaka kuendelea kusoma/kusikiliza. Baadhi ya hadithi huishia kwa taharuki na kuilazimisha hadhira yake ijikamilishie au ibaki ikijiuliza maswali. Suspense
- Sadfa - Sadfa ni kugongana kwa vitendo viwili vinavyohusiana kana kwamba vilikuwa vimepangwa, japo havikuwa vimepangiwa. Coincidence
- Kisengere Nyuma - Mwandishi 'hurudi nyuma' na kuanza kusimulia kisa kilichokuwa kimetendeka kabla ya alichokuwa akisimulia. Aidha, mwandishi hubadilisha wakati wa masimulizi na kuwa wakati wa kisa hicho. Hutumika sana kuonyesha mhusika anapokumbuka kitu, au kutupatia msingi wa jinsi mambo yalivyoanza. Mbinu Rejeshi. Flashback
- Kisengere Mbele - Mwandishi anapobadilisha wakati na kusimulia mambo yatakavyokuwa siku za usoni; au kutumia lugha isiyo moja kwa moja kutabiri yatakayojiri. Utabiri. Foreshadow
- Njozi au Ndoto - Mwandishi hutumia ndoto kutabiri jambo litakalofanyika au kufumbua jambo lililokuwa limefumbwa.
- Upeo wa Juu - Ni sehemu ya hadithi ambayo matukio yanafanyika kulingana na mapenzi ya hadhira au msomaji. Climax
- Upeo wa Chini - Ni sehemu ya hadithi ambayo matukio yanafanyika kinyume na mapenzi ya hadhira au msomaji. Aghalabu upeo wa chini hutokea baada ya upeo wa juu. anti-climax
- Nyimbo - Nyimbo na/au mashairi yanaweza kutumika katika hadithi kwa madhumuni mbalimbali.