Sajili ya Michezoni
Lugha ya michezoni hutumiwa wakati wa mashindano ya michezo kama vile kandanda, ukimbiaji n.k Hii inaweza kuwa lugha ya watangazaji/wasimulizi wa mchezo, watazamaji, mashabiki au wachezaji.
Sifa za Lugha ya Michezoni
- Hutumia msamiati wa kipekee unaohusu michezo kama vile mpira, goli, mchezaji
- Huchanganya ndimi na kuingiza maneno ya lugha nyingine kama vile Kiingereza. mfano 'goal!!!'
- Ni lugha ambayo hutumia vihisishi na mshangao kwa wingi
- Sentensi nyingi katika lugha hii huachwa bila kukamilika hasa hali inapobadilika uwanjani
- Husimuliwa kwa haraka haraka ili kuambatana na kasi ya mchezo
- Ni lugha yenye sifa na na chuku kwa mfano msimulizi anaposimulia sifa za mchezaji fulani
- Hutumia misimu kama vile 'wametoka sare'
- Hutumia kwa ya kulinganisha ili kuelezea matokeo ya mechi k.m 'walitoka mbili kwa nunge'
- Ni lugha yenye kukariri (kurudia rudia) hasa mchezaji anapoumiliki mpira kwa muda mrefu au mwanariadha fulani anapoelekea kushinda katika mbio.
- Huwa na sentensi fupi fupi
Mfano wa Sajili ya Michezoni
Nakwambia ndugu msikilizaji hapa mambo yamechacha kwelikweli. Hawa wachezaji wa Manyuu hawacheki na watu leo. Wameamua kuishambulia timu ya Cheusi bila huruma. Kumbuka kwamba hii ni mara yao ya... Lo! Anauchukua mpira pale, mchezaji nambari tisa... Matiksta. Matiksta, Matiksta na mpira. Anaucharazacharaza pale. Anamwangalia mwenzake. Anaupiga mpira kwa kichwa pale! Lo! Mwenzake anaukosa. Akiushika mpira pale ni mchezaji wa timu ya Cheusi, Romana. Romana, Romana anaelekeza mpira kwenye lango la Manyuu. Anaupiga mpira kwa nguvu! Lo! Hatari sana. Hatari sana katika lango la Manyuu. Hatari! hatari! Gooooaaaaaal! Noooo ooh! Wameukosa! Goal keeper ameudaka mpira huo. Pole sana wachezaji wa ... Mlinda lango anaupiga mpira huo kwa hasira. Juu kabisa. Anauchukua pale nambari saba, Saruta. Huyu ni mchezaji machahari sana. Mwaka uliopita, alipewa tuzo la mchezaji bora wa mwaka. Ananyang'anywa na mchezaji mwingine hapa. Wanakabiliana kidogo. Huyu mchezaji anaupiga mpira kwa mguu wa kushoto. Lo! Mpira umekuwa mwingi na ukatoka nje.
Mashabiki wa timu hizi mbili wanasubiri kwa hamu na ghamu kutambua ni nani atakayeibuka mshindi. Katika mechi zilizotangulia, timu hizi zimekuwa zikitoka sare. Lakini leo lazima mshindi atapatikana. Hawa ni fahali wawili. Kumbuka kwamba unapata matangazo haya moja kwa moja kupitia idhaa yako uipendayo, redio nambari moja kote nchini... Mpira unarudishwa uwanjani. Akienda kuurusha pale ni...