Vipera vya Ngano
Tunaweza kuainisha ngano kulingana na vipengele vifuatavyo:- Wahusika => k.v khurafa, hekaya, mighani, mazimwi,
- Maudhui => k.v usuli, visasili, mtanziko
AINA | MAELEZO KWA UFUPI |
Khurafa | hadithi ambazo wahusika ni wanyama. |
Hekaya | mhusika mmoja (k.v sungura) huwa mjanja kuliko wenzake |
Usuli (Visaviini) | huelezea chanzo cha jambo au hali fulani |
Visasili | huelezea asili au chimbuko la jamii au mambo ya kiada k.v mauti, ndoa, tohara n.k. |
Mighani (Visakale) | hadithi za mashujaa |
Mazimwi | huwa na wahusika majitu au mazimwi |
Mtanziko | humwacha mhusika katika hali ya kutojua chaguo linalofaa. Kila achagualo lina matukio mabaya. |
Sifa za Ngano
- Huwa na mianzo maalumu
- Paukwa! Pakawa!
- "Hadithi! Hadithi!" - "Hadithi Njoo!"
- Hapo zamani za kale...
- Huwa na miishio maalum
- Hadithi yangu yaishia papo!
- ...wakaishi kwa raha mustarehe.
- Huwa na funzo fulani ambalo aghalabu hutajwa mwishoni mwa hadithi.
- Masimulizi yake huwa kwa wakati uliopita
- Husimuliwa kwa lugha ya natharia
- Huwa na wahusika ambao wanaweza kuwa binadamu, wanyama, miungu, mashetani au vitu visivyo hai
- Huhusisha mbinu nyingine za fasihi simulizi kama vile
- Nyimbo - kuburudisha, kuamsha hadhira, kupitisha ujumbe
- Methali - kutoa funzo
- Misemo - kupamba lugha
- Vitendawili na mafumbo - kushirikisha hadhira katika masimulizi
- Hutumia mbinu ya takriri ili kusisitiza ujumbe kwa kurudiarudia maneno, matukio au nyimbo
- Hutumia tamathali za lugha kama vile tashbihi, tashihisi, chuku, tanakali za sauti ili kupamba masimulizi n.k
- Huwa na muundo rahisi wenye mwanzo, kati na mwisho.
- Ufanisi wake hutegemea mbinu za mtambaji k.v ishara-uso na ubunifu wake jukwaani.
- Sehemu fulani zinaweza kubadilishwa kulingana na hadhira
Umuhimu wa Ngano
- Kuhifadhi au kurithisha mali ya jamii
- Kuunganisha na kukuza ushirikiano miongoni mwa jamii
- Kuelemisha au kutoa mafunzo kuhusu mambo fulani
- Kukuza maadili mema
- Kuonya, kuelekeza, kuhimiza na kunasihi
- Kuburudisha hadhira. Hadithi nyingi huwa na visa vya kusisimua na kuburudisha.
- Kupitisha muda haswa watoto wanaposubiri chakula kiive
Sifa za Mtambaji wa Hadithi
Msimulizi wa hadithi pia huitwa mtambaji, fanani au mganaji.- Huwa mchangamfu na mcheshi kwa hadhira yake ili kuwafanya wapendezwe na hadithi
- Anafahamu utamaduni wa jamii yake.
- Anaifahamu hadhira yake vizuri na kusimulia kulingana na mapendeleo yao. wasichana au wavulana? vijana au wazee?
- Huwa na uwezo wa ufaraguni - uwezo wa kubadilisha sehemu fulani za sanaa bila kujifunga na muundo asilia.
- Mwenye kumbukumbu nzuri - uwezo wa kukumbuka
- Mwenye uwezo wa kuigiza kwa kutumia viungo vyake, uso (ishara-uso) na sauti(kiimbo)
- Mwenye uwezo wa kujenga taharuki kwa kusita kidogo ili kuvuta nadhari ya hadhira yake.
- Hushirikisha hadhira yake katika nyimbo n.k
- Mlumbi hodari na mkwasi wa lugha.