Viwakilishi (W)
Viwakilishi vya Nomino ni maneno yanayotumika badala ya nomino. Kiwakilishi hakiwezi kuambatanishwa na nomino inayorejelewa.
Aina za Viwakilishi
Viwakilishi vya Nafsi
Viwakilishi hivi hutumika kwa niaba ya nafsi kwa umoja na kwa wingi.
NAFSI | UMOJA | WINGI |
Nafsi ya Kwanza | Mimi | Sisi |
Nafsi ya Pili | Wewe | Ninyi/Nyinyi |
Nafsi ya Tatu | Yeye | Wao |
- Sisi tuliwatangulia nyinyi kufika hapa.
- Mimi si mjinga kama vile yeye anavyofikiria
Viwakilishi Viashiria
Viwakilishi viashiria (vionyeshi) hutumika badala ya nomino kwa kutumia kuonyesha nomino inayorejelewa bila kuitaja.
- Hiki hakina maandishi yoyote.
- Hao hawajui tofauti ya viwakilishi na vivumishi
- Tumekuja hapa ili kuwaburudisha kwa nyimbo tamu tamu.
Viwakilishi Visisitizi
Husisitiza nomino inayowakilishwa kwa kurudiarudia kiashiria chake.
- Zizi hizi ndizo zilizovunjika wiki jana
- Yule yule aliyekamatwa juzi, ameiba tena.
Viwakilishi vya Sifa
Husimama badala ya nomino kwa kurejelea sifa yake.
- Vyekundu vimehamisha
- Warembo wamewasili.
- Kitamu kitaliwa kwanza.
Viwakilishi vya Idadi
Hutumika kusimama badala ya nomino kwa kurejelea idadi yake.
a) Idadi Kamili- hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
- Wawili wamepigwa risasi polisi leo jioni.
- Alimpatia mtoto wake hamsini kununua chakula
b) Idadi Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
- Tutazungumza na wachache kabla ya kuanzisha maonyesho yetu.
- Kadhaa zimeripotiwa kupotea.
Viwakilishi Viulizi
Viwakilishi viulizi hutumika kwa niaba ya nomino katika kuulizia swali.
Baadhi ya viwakilishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli
- Vingapi vinahitajika? - kuulizia idadi
- Zipi zimepotea?
Kunavyo viwakilishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
- Gani imefunga bao hilo?
- Wapi hapana majimaji?
- Yule mvulana alikupatia nini?
- Uliongea naye vipi? - kuulizia namna
Viwakilishi Vimilikishi
Viwakilishi hivi hurejelea nomino kwa kutumia vimilikishi.
- Kwetu hakuna stima.
- Lake limekucha.
- Zao zimeharibika tena
Viwakilishi Virejeshi (O-Rejeshi)
Hutumia O-rejeshi kurejelea na kusimamia nomino
- Ambalo lilipotea limepatikana.
- Ambaye hana mwana, aeleke jiwe
Viwakilishi Vya A-Unganifu
Huwakilishi nomino kwa kutaja kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino nyingine
- Cha mlevi huliwa na mgema
- Za watoto zitahifadhiwa.