Nomino (N)
Nomino ni maneno ambayo ni majina ya watu, vitu, hali n.k. Kuna nomino za kawaida na nomino za kipekee miongoni mwa aina nyingine za nomino.
Aina za Nomino
Kunazo aina mbalimbali za nomino katika lugha ya Kiswahili.
- Nomino za Kipekee
- Nomino za Kawaida
- Nomino za Jamii/Makundi
- Nomino za Kitenzi-Jina
- Nomino za Dhahania
- Nomino za Wingi
Nomino za Kawaida
Haya ni majina ya kawaida yanayoweza kutumiwa kurejelea vitu mbalimbali, watu, wanyama, mahali na kadhalika. Nomino hizi zinaweza kuwa katika umoja au wingi kulingana na ngeli yake.
k.m: nyumba, mbuzi, daktari, soko, kalamu, jua
Nomino za Kipekee
Haya ni majina maalum ya watu, mahali, bidhaa, kampuni, na kadhalika. Herufi ya kwanza ya nomino hizi huwa ni herufi kubwa. Nomino za kipekee haziwezi kubadilika, na hivyo basi hazina wingi.
k.m: Tanzania, Nairobi, Anita, Gafkosoft, Athi, Kimbo,
Nomino za Jamii
Nomino za jamii hurejelea kundi la vitu au wanyama, kwa ujumla. Aghalabu vitu vinavyorejelewa hutokea kwa makundi ya vitu mbili au zaidi. Nomino hizi hutumia wingi tu tunaporejelea makundi zaidi ya moja.
k.m: jozi la viatu, umati wa watu, bustani la maua, bunga la wanyama
Nomino za Wingi
Nomino hizi hurejelea vitu ambavyo hutokea kwa wingi na haziwezi kuhesabiwa. Vitu kama hivyo hutumia aina nyingine ya vipimo ili kurejelea kiasi chake. Nomino za wingi hazina umoja.
k.m: maji, maziwa, changarawe, pesa, nywele
Nomino za Vitenzi Jina
Nomino hizi huundwa kutokana na vitenzi kwa kuongeza kiungo KU mwanzoni mwa mzizi wa kitenzi.
k.m: kulima, kuongoza, kucheza, kulala
Nomino za Dhahania
Haya ni majina ya hali au vitu ambavyo havionekani wale haviwezi kushikika.
k.m: upendo, furaha, imani, elimu, ndoto, mawazo, maisha, usingizi