Msamiati wa Mapambo

Mapambo ni vitu vinavyovaliwa na watu ili kujirembesha; kuwafanya wavutie machoni pa watu wengine;

Mifano

 1. bangili:
  ni pambo la duara linalovaliwa mkononi na wanawake.
 2. herini:
  ni pambo linalovaliwa kwenye ndewe la sikio.
 3. hina:
  ni rangi nyekundunyekundu inayopakwa miguuni na mikononi mwa wanawake.
 4. kago:
  ushanga unaovaliwa kiunoni
 5. kanta:
  ni rangi nyeusi inayopakwa kwenye mvi (nywele nyeupe) ili nywele zionekana kama nyeusi, hasa na wale wasiopenda uzee.
 6. keekee:
  ni pambo linalovaliwa na wanawake mkononi kama kikuku au bangili.
 7. kigesi:
  bangili/kikuku kinachovaliwa na wanawake miguuni.
 8. kikuku:
  pambo la duara linalovaliwa mkononi au mguuni.
 9. kipini:
  pambo linalovaliwa puani (sehemu ya juu)
 10. kishaufu:
  hili ni pambo la duara linalovaliwa puani (sehemu ya chini).
 11. mafuta:
  ni kitu kioevu kinachopakwa mwilini kwa makusudi ya kulainisha ngozi na kunukia vizuri.
 12. marashi:
  haya ni kifurushi, maji au mafuta yanayonukia vizuri yanayoundwa kwa mawaridi na kemikali nyingine yanayopakwa mwilini hasahasa kwapani.
 13. mkufu:
  ni kitu chembamba kama mnyororo kinachoundwa kwa madini kama dhahabu, fedha n.k kinachovaliwa shingoni.
 14. mshipi:
  ni mkanda unaovaliwa kiunoni.
 15. ndewe:
  ni tundu linalotobolewa kwenye sehemu ya chini ya sikio ili kuvaliwa mapambo ya sikioni.
 16. ndonya:
  ni tundu linalotobolewa katika sikio na mdomo wa juu au mdomo wa chini
 17. nembo:
  ni chale zinazochanjwa usoni au kwenye sehemu nyingine za mwili. Nembo zilitumika kuonyesha kubaleghe(kuvunja ungo) kwa wasichana; kubainisha kabila au kuonyesha urembo tu.
 18. njuga:
  kengele ndogondogo zinazovaliwa shingoni, miguuni na mikononi hasa wakati wa kucheza ngoma za kitamaduni.
 19. nti:
  ni vijiti vidogo vinavyovaliwa na wanawake masikioni baada ya kutoga ndewe.
 20. nyerere:
  ni uzi mwembamba wa madini unaovaliwa mikononi na miguuni.
 21. nywele bandia:
  ni nywele za kununua zinazovaliwa na kina dada ili kujiongezea urembo.
 22. pete:
  pambo la madini la duara linalovaliwa kidoleni.
 23. poda:
  ni rangi nyeupe, laini itumiwayo na wanawake kujipaka.
 24. rangi ya kucha:
  ni rangi inayopakwa kwenye kucha na wasichana
 25. rangi ya midomo:
  ni rangi nyekundunyekundu inayopakwa kwenye midomo na wanawake.
 26. saa:
  kifaa cha kupimia wakati kinachovaliwa mkononi kama pambo.
 27. tai:
  nguo/kitambaa kilichoundwa ili kuvaliwa shingoni juu ya shati haswa wakati wa shughuli rasmi
 28. taji:
  kofia inayovaliwa na wafalme, watawala au washindi kuashiria cheo chao au ushindi wao.
 29. ukaya:
  nguo au kitambaa kinachovaliwa kukinga sehemu ya mdomo hasa na wanawake Waislamu.
 30. usinga:
  nywele za farasi au nyumbu zinazovaliwa mkononi bangili.
 31. wanja:
  ni rangi nyeusi ya majimaji au ungaunga inayotumika na wanawake kupaka machoni, usoni, mikononi na hata miguuni.