Viunganishi (U)

Viunganishi ni maneno yanayoutumika kuunganisha, kulinganisha au kuonyesha uhusiano wa dhana mbili au zaidi.

Aina za Viunganishi

Zifuatazo ni aina mbalimbali za viunganishi kulingana na matumizi yake

Kuonyesha Umilikaji

A-Unganifu Kiatu cha Mzee Sakarani kimepasuka.
KWA (umilikaji wa mahali) Mbinguni kwa kuna makao mengi.

Kujumuisha

na Baba, mama na watoto huunda familia kamili.
pamoja na Mwizi aliiba runinga pamoja na redio
fauka ya, licha ya Fauka ya mapigo yote, Kafa alikatakatwa kwa kisu.
zaidi ya, juu ya Unataka nini tena zaidi ya mema yote niliyokutendea?
pia, vilevile Alimpiga mkewe na bintiye vilevile
mbali na Mbali na hayo nitakujengea nyumba ya kifahari.
aidha Keti akitoka shuleni atapika. Aidha atampelekea nyanya sukuma wiki.
wala (kukanusha) Ndege wa angani hawalimi wala hawapandi.

Kutofautisha

lakini, ila Ongea nayeilausimwambie mipango yetu.
bila Tasha aliondoka bila kusema lolote.
bali Sitawaacha kama mayatima bali nitawatumia msaidizi.
kinyume na, tofauti na Jana kulinyesha kinyume na utabiri wa hali ya hewa.
ingawa, ingawaje Nitamtembelea ingawa sijui nitamwambia nini.
japo, ijapokuwa Nakuomba upokee nilichokileta japo ni kidogo sana.
ilhali Fungo zimepotea ilhali zilikuwa zimewekwa vizuri.
minghairi ya Waliendelea kutenda dhambi minghairi ya kuhubiriwa kanisani.
dhidi ya Vita dhidi ya gonjwa hilo vingali vinaendelea.

Kuonyesha Sababu

ili Hanna aliumizwa ili asikumbuke aliyoyaona.
kwa, kwa vile Emili alinyamaza kwa vile kugombana na rafikize.
kwa maana, kwa kuwa Aria alipigwa na butwaa kwa maana mpenzi wake aligeuka kuwa mwalimu wake.
kwani Melisa alijificha kwani hakutaka kuonekana na Spensa.
kwa minanjili ya Chali alitembea mwendo huo wote kwa minanjili ya kuongea na Katosha.
maadam Wanawake katika familia hiyo hawali maini maadam mama mkongwe alilaani maini katika familia hiyo.
madhali Madhali sote tuko hapa, tunaweza kuanzisha mkutano mapema

Kuonyesha Matokeo

basi, hivyo basi Umekula ng'ombe mzima, hivyo basi huna budi kumalizia mkia.
kwa hivyo Alipatikana na makosa ya kumnajisi bintiye, kwa hivyo akahukumiwa miaka kumi gerezani.
ndiposa Mama Kelele alipenda kuongea sana, ndiposa wakamkata midomo.

Kulinganisha

kama, sawa na Kunywa pombe ni kama kujichimbia kaburi mwenyewe.
kulingana na Mwalimu Makunza hafanyi kazi kulingana na maadili ya shuleni.
kuliko, zaidi ya Talia ni mfupi kuliko Nuru
vile Mganga Daimoni hutibu vile alivyofunzwa na Mganga Kuzimu.

Kuonyesha Kitu kimoja kama sehemu ya kingine

kati ya Vitatu kati ya vitabu hivi vimepigwa marufuku.
miongoni mwa Miongoni mwa walioachiliwa, ni Ngiri na Mende.
baadhi ya Baadhi ya wasichana kutoka Vikwazoni hawaheshimu miili yao.
mojawapo Mojawapo ya maembe uliyochuma yameoza.

Kuonyesha Kitu kufanyika baada ya kingine

kisha Soma mfano huu kisha usome sentensi ifuatayo.
halafu Alichukua kisu halafu akatokomea gizani.

Kuonyesha Kitu kufanyika badala ya kingine

badala ya Mapepo yalimchukua Shakawa badala ya bintiye
kwa niaba ya Mama Roga alitoa hotuba kwa niaba ya mumewe.

Kuonyesha Uwezekano

labda, pengine Sina pesa leo, labda uje kesho.
ama, au Ama Anita au Katosha anaweza kuja.
huenda Huenda kesho ikifika, Mungu atende miujiza.

Kuonyesha Masharti

bora, muradi Sitakuuliza bora tu usichelewe.
ikiwa, iwapo Ikiwa huna jambo muhimu la kusema, nyamaza.