Kukanusha

Kukanusha ni kukataa au kukana kauli.

Mara nyingi tunapokanusha, tuanaongeza kiambishi 'HA-' mwanzoni mwa kitenzi. Hata hivyo, kiambishi hicho hubadilika katika nafsi ya kwanza na ya pili umoja. Angalia jedwali lifuatalo.

Kukanusha Nyakati Mbalimbali

Kukanusha Wakati Uliopita (LI) => 'KU'

 • Kajuta alimpigia kura. - Kajuta hakumpigia kura.
 • Nilikupa nafasi yako. - Sikukupa nafasi yako.

Kukanusha Wakati Timilifu (Uliopita Muda Mfupi) (ME) => 'JA'

 • Maziwa ya nyanya yamemwagika. Maziwa hayajamwagika.
 • Viwete wametembea - Viwete hawajatembea.

Kukanusha Wakati Uliopo (NA) => '-I'

 • Unasoma sentensi ya kwanza. - Husomi sentensi ya kwanza.
 • Zinafanana na nyota. - Hazifanani na nyota.

Kukanusha Wakati Ujao (TA) => 'TA'

 • Jua litawaka sana. - Jua halitawaka sana.
 • Watakaribishwa kwenye malango ya lulu. - Hawatakaribishwa kwenye malango ya lulu.

Kukanusha Wakati wa Mazoea (HU) => '-I'

 • Polisi wa jiji kuu huchukua hongo. - Polisi wa jiji kuu hawachukui hongo.
 • Bendera hufuata upepo. - Bendera haifuati upepo.

Kukanusha Wakati Usiodhihirika (A) => '-I'

 • Anita ampenda Kaunda. - Anita hampendi Kaunda.
 • Chema chajiuza, kibaya chajitembeza. - Chema hakijiuzi, kibaya hakijitembezi.

Kukanusha KI ya Masharti (KI) => 'SIPO'

 • Ukimwadhibu mtoto, atapata adabu njema. - Usipomwadhibu mtoto hatapata nidhamu..
 • Bei yake ikishuka, nitainunua. - Bei yake isiposhuka, sitainunua.

Kukanusha PO ya Wakati (PO) => 'SIPO'

 • Uamkapo asubuhi ndugu yangu mshukuru Mungu. - Usipo amka asubuhi ndugu yangu usimshukuru Mungu.
 • Mtoto aliapo mnyonyeshe. - Mtoto asipo lia usimnyonyeshe

Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGE) => 'SINGE'

 • Ningekuwa nakupenda ningekwambia mapema. - Nisingekuwa nakupenda nisingekwambia mapema.
 • Zingekuwa nyingi, wangeziiba. - Zisingekuwa nyingi, wasingeziiba.

Kukanusha Hali ya Uwezekano (NGALI) => 'SINGALI'

 • Khadija angalisoma kwa bidii angalikuwa na cheo kikubwa. - Khadija asingalisoma kwa bidii asingalikuwa na cheo kikubwa
 • Yangalikuwa mabivu yangalianguka yenyewe. - Yasingalikuwa mabivu yasingalianguka yenyewe

Kukanusha Amri/Agizo (-a/-e) => 'SI'

 • Peleka kikapu hiki kwa nyanya. - Usipeleke kikapu hiki kwa nyanya.
 • Chakula kiliwe. - Chakula kisiliwe.
 • Mpende adui yako. - Usimpende adui yako.
 • Waambieni watu wa mataifa yote. Msiwaambieni watu wa mataifa yote.

Kukanusha Viunganishi vya Kujumuisha (NA, KA) => 'WALA'

 • Bafi alikuzaba kofi na kukupiga teke. - Bafi hakukuzaba kofi wala hakukupiga teke.
 • Mama amepika chakula tukala pamoja. - Mama hajapika chakula wala hatujala pamoja.