Vivumishi (V)
Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na nomino.
Aina za Vivumishi
Vivumishi vya Sifa
Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k
- Yule mama mweusi hupika chakula kitamu.
- Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.
- Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni
Vivumishi Vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inamiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi huundwa kulingana na nafsi mbalimbali ( -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao).
- Nitatumia talanta zangu kwa manufaa ya taifa letu.
- Aliweka kitabu chako sebuleni mwako
- Katosha amepata nguo yake miongoni katika sanduku lao.
Vivumishi vya Idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi.
a) Idadi Kamili
hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
k.m: tatu, mbili, kumi
- Msichana mmoja amewauwa nyoka wawili
- Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu
b) Idadi Isiyodhihirika
huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
- Watu wachache waliohudhuria mazishi ya Kajuta walikula chakula kingi sana.
- Baba yao alikuwa mateka kwa miaka kadhaa.
Vivumishi Visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria
- Jahazi lili hili
- Wembe ule ule
- Ng'ombe wawa hawa
Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.
Karibu | hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale |
Mbali kidogo | hapo, huyo, hiyo, hicho |
Mbali zaidi | pale, lile, kile |
- Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule
- Jani hili la mwembe limekauka
- Tupa mpira huo
Viwakilishi Viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngel
- Ni walimu wangapi wamefukuzwa? - kuulizia idadi
- Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu?
Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
- Unazungumza kuhusu kipindi gani?
- Je, mmefika mahali wapi? - kuulizia mahali
Vivumishi Virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino.
- Msichana ambaye alikuja ni Sheila
- Sauti ambayo uliisikia ilikuwa ya Mzee Kasorogan
Vivumishi vya KI-Mfanano
Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine. Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI.
- Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimasikini
- Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu
- Bi Naliza huvulia mavazi ya kifalme.
Vivumishi Vya A-Unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo. Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu, kisha nomino
- Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri
- Chai ya daktari imemwagika