Viambishi
Angalia: Uainishaji wa Neno
Kuna aina mbili kuu za viambishi:
- Viambishi Awali
- Viambishi Tama
Viambishi Awali
Viambishi hivi hutokea kabla ya mzizi ya neno / shina la kitenzi. Kuna aina kadhaa za viambishi hivi kama vile viambishi viwakilishi vya nafsi, ngeli, mahali, wakati, hali n.k
Viambishi Viwakilishi vya Ngeli
Hizi ni silabi zinazowakilisha ngeli katika neno. Mfumo wa ngeli unaokubalika hutumia viambishi hivi kubainisha ngeli mbali mbali.
k.m:
- a-me-avy-a => kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya A-WA(umoja)
- zi-ta-pasuk-a => kiambishi kiwakilishi cha ngeli I-ZI wingi
- ki-li-pote-a => kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI(umoja)
- ya-na-angaz-iw-a => kiambishi kiwakilishi cha ngeli ya LI-YA(wingi)
Viambishi Viwakilishi vya Nafsi
hivi ni viambishi ambavyo huonyesha nafsi katika neno. Kuna aina mbili za viambishi viwakilishi vya nafsi:
a) Viambishi Viwakilishi vya Nafsi ya Mtendaji/Mtenda
=> Hutumika kuonyesha aliyefanya kitendo katika neno. Kama viambishi vya Ngeli ya Mtendaji, viambishi hivi ndivyo vinavyotangulia viambishi vingine katika kitenzi.
NAFSI | UMOJA | WINGI | MFANO |
YA KWANZA | NI | TU | ni-na-andik-a, tu-li-shind-a |
YA PILI | U | M | u-me-kasir-ik-a, m-na-pig-w-a |
YA TATU | A | WA | a-li-simam-a, wa-ta-p-ew-a |
b) Viambishi Viwakilishi vya Nafsi ya Mtendewa/Mtendwa => Hutumika kuonyesha nafsi ya aliyeathirika na kitendo katika neno.
Kama viambishi viwakilishi vya ngeli ya mtendewa, mara nyingi viambishi hivi huwekwa punde kabla ya shina la kitenzi.
Viambishi viwakilishi vya mtendewa ni sawa na viambishi viwakilishi vya mtendaji isipokuwa:
NAFSI YA MTENDEWA | KIAMBISHI | MFANO |
YA PILI UMOJA | KU | zi-me-ku-fik-i-a |
YA PILI WINGI | M, MU, WA | ni-na-wa-tum-a |
YA TATU UMOJA | M | ni-ta-m-tambu-a |
Viambishi Viwakilishi vya Wakati/ Hali
Hivi ni viambishi ambavyo vinapowekwa kabla ya shina la kitenzi, vinatufahamisha wakati kitendo hicho kilipofanyika.
Viambishi hivi ni:
KIAMBISHI | HUWAKILISHA: | MFANO |
LI | wakati uliopita | kili-chom-ek-a |
ME | wakati timilifu (uliopita muda mfupi) | zi-me-anguk-a |
NA | wakati uliopo | tu-na-ku-subir-i |
TA | wakati ujao | wa-ta-ni-ju-lish-a |
HU | wakati wa mazoea | hu-som-e-a |
A | wakati usiodhihirika | a-tu-pend-a |
KA | wakati usiodhihirika | zi-ka-teket-e-a |
PO | PO ya wakati | a-li-po-wasil-i |
KI | KI ya masharti | ni-ki-zi-angali-a |
Viambishi Viwakilishi vya Kukanusha Wakati
Viambishi hivi hutumika kukanusha kitenzi katika sentensi kulingana na wakati au hali
KIAMBISHI | HUKANUSHA: | MFANO |
KU | wakati uliopita | haku-ingi-a |
JA | wakati timilifu (uliopita muda mfupi) | si-ja-ku-uliz-i-a |
-I* | wakati uliopo na wa mazoea | ha-som-i |
TA | wakati ujao | ha-ki-ta-maliz-ik-a |
Tanbihi:
- Tunapokanusha wakati uliopo, wakati wa mazoea na wakati usiodhihirika, tunatumia kiambishi kiishio(I)
badala ya kutumia kiambishi tamati.
k.m:si-ku-ju-i, ha-pat-ik-an-i
Viambishi Viwakilishi vya Kukanusha Nafsi
Tunapokanusha kitenzi, kiambishi cha kwanzwa hubadilika kulingana na nafsi.
KIAMBISHI | MATUMIZI | MFANO |
SI | nafsi ya kwanza | si-ku-wa-on-a |
HU | nafsi ya pili | hu-ni-faham-u |
HA | nafsi ya tatu | ha-ta-chuku-a |
Viambishi Virejeshi vya Ngeli
Hurejelea ngeli ya mtendewa au mtendwa na hutumika hasa katika vishazi tegemezi (vyenye o - rejeshi)
k.m:
- wa-li-cho-nitum-i-a => kiambishi kirejeshi cha ngeli ya KI-VI
- ni-ta-ka-ye-m-salim-i-a => kiambishi kirejeshi cha ngeli ya A-WA
- u-li-ko-ji-fich-a => kiambishi kirejeshi cha ngeli ya mahali KU
- tu-li-po-pa-safish-a => kiambishi kirejeshi cha ngeli ya mahali PO
Viambishi Tama
Viambishi tama hutokea baada ya shina la kitenzi na hutumika kutuarifu kauli au myambuliko wa kitenzi hicho.
Viishio
Katika kauli ya kutenda, vitenzi vyenye asili ya Kibantu huishia kwa sauti "-a". Kwa mfano: a-na-omb-a, tu-li-zo-andik-a
Tanbihi: Tunapokanusha vitenzi hivi vyenye asili ya Kibantu katika wakati uliopo na wakati wa mazoea kiishio "-a" hubadilika na kuwa "-i" ''' Kwa mfano: ' Ha-pat-ik-an-i, Si-ku-ju-i ''
Vitenzi vyenye asili ya kigeni huchukua viishio tofauti kama vile e, i na u katika kauli ya kutenda. Kwa mfano: ha-wa-ja-tu-jib-u, a-na-tu-subir-i, ni-me-ku-sameh-e
Hata hivyo katika kauli nyinginezo (isipokuwa kauli ya kutenda) vitenzi hivi vya kigeni huchukua kiishio "a". k.m harib-ik-a, tu-me-jib-iw-a
Viambishi Viwakilishi vya Kauli ya Kitenzi
Hubadilika kulingana na mnyambuliko wa kitenzi.
KAULI | KIAMBISHI | MFANO |
KUTENDEA | e, i | omb-e-a, pig-i-a, |
KUTENDEANA | ean, ian | omb-ean-a, pig-ian-a, |
KUTENDWA | w | som-w-a |
KUTENDEWA | ew, iw | omb-ew-a, pig-iw-a |
KUTENDEKA | ek | pend-ek-a |
KUTENDESHA | esh, ez, ish, iz | kom-esh-a, ing-iz-a |
KUTENDANA | an | finy-an-a |
Kwa mifano zaidi, angalia mnyambuliko wa vitenzi.