Muundo wa Sentensi
Kiima, Kiarifa, Shamirisho na Chagizo
Sentensi huwa imeundwa na maneno mbalimbali. Vijenzi hivi vya sentensi ni Kiima, Kiarifa, Shamirisho na Chagizo
Angalia:
- Aina za Sentensi => Sahili, Changamano, Ambatano
- Virai na Vishazi
- Uchanganuzi
Kikundi Tenzi(KT) na Kikundi Nomino(KN)
Hizi ndizo sehemu mbili kuu katika sentensi. Kila kundi kikundi kinaweza kuwa na maneno mbalimbali. Tutayachangua haya zaidi katika uchanganuzi wa sentensi.
Kikundi Nomino (Kiima): KN
Ni sehemu wa sentensi yenye nomino. Pia kikundi nomino kinaweza kushirikisha kikundi kivumishi au kishazi tegemezi. k.m:
- '_'Safari'_' zawa salama bila misukosuko.
- '_'Wanafunzi waliokuwa wametoroka shuleni'_', wamekamatwa na kuadhibiwa.
- '_'Matunda matamu'_' huvutia sana.
Kikundi Tenzi (Kiarifa): KT
Ni sehemu ya sentensi yenye kitenzi. Licha ya kitenzi, kikundi tenzi kinaweza kushirikisha kikundi kielezi au kikundi kivumishi. Aidha, kikundi tenzi kinaweza kuwa na kikundi nomino kama shamirisho kipozi au kitondo.
k.m:- Mvua '_'inarutubisha vitu vyote.'_'
- Dunia '_'huzunguka jua.'_'
- Madawati yaliyokuwa yamechafuliwa '_'yamesafishwa.'_'
Shamirisho
Shamirisho ni mtendwa au mtendewa katika sentensi. Ni sehemu ya sentensi inayowakilisha kitu kilichofanyiwa kitu. Kuna aina tatu za shamirisho.
Shamirisho Kipozi - (direct object)
Ni sehemu inayowakilisha nomino inayopokea kitendo hicho moja kwa moja. Mtendwa
- Nyanya aliwasalimia '_'wajukuu wake.'_'
- Bustani la Kuzimu linawatisha '_'watu wengi.'_'
- Rita alimwandikia kakake '_'barua'_' kwa kalamu nyeusi.
Shamirisho Kitondo - (indirect object)
Huwakilisha ambayo kitendo kinafanywa kwa ajili yake au kwa niaba yake. Mtendewa
- Mama aliwapikia '_'watoto'_' ugali tamu.
- Bibi anawasimulia '_'wasichana wadogo'_' hadithi za kikale.
- Rita alimwandikia '_'kakake'_' barua kwa kalamu nyeusi.
Shamirisho ala kitumizi
Hurejelea ala au kifaa kinachotumika kutekeleza kitendo hicho
- Wetu wengine huvuna mahindi '_'kwa panga.'_'
- Mchungaji Thabiti alikufa '_'kwa maji.'_'
- Rita alimwandikia kakake barua '_'kwa kalamu'_' nyeusi.
Chagizo
Hutuelezea zaidi kuhusu kiima, kiarifa au shamirisho. Aghalabu chagizo huwa kielezi au kivumishi.
- Mama M alimvalisha bintiye mavazi '_'ya kupendeza'_'.
- Mumbe ni msichana '_'hodari sana'_'.
- Kinyonga hupendelea kutembea '_'polepole.'_'
- Rita alimwandikia kakake barua kwa kalamu '_'nyeusi.'_'