Vihisishi (I)
Vihisishi ni maneno yanayotumika kuonyesha hisia kama vile hasira, furaha, mshangao, kusifia, kushangilia n.k. Vihisishi hutambulishwa katika sentensi kwa kuambatanishwa na alama ya mshangao (!). Kihisishi kimoja kinaweza kutumika kutoa hisia tofauti kulingana na muktadha.
Mifano ya Vihisishi
Ifuatayo ni baadhi ya mifano ya maneno yanayotumika kuonyesha hisia. Hata hivyo, maneno mengine yoyote yanaweza kutumika kama vihisishi, kulingana na mukhtadha. k.v Potelea mbali!
Kihisishi | Mfano katika Sentensi | Hisia |
Lo! | Lo! Maajabu ya Musa haya! | mshangao |
Salaale!, Masalaale! | Salaale! Angalia watu wote hawa waliofika mahali hapa! | mshangao |
Kumbe! | Nilidhani wewe ni rafiki yangu. Kumbe! | mshangao |
Po! | Sijawahi kuona kijana mjeuri kama wewe. Po! | hasira |
Ng'o! | Omba msamaha utakavyo, lakini unachoka bure. Ng'o! | kiburi |
Hata! | Bwanake hakumwachia chochote! Hata! | kusifia, kupuuza |
Akh!, Aka! | Mtoto mpumbavu huyu! Akh! | hasira, kukashifu |
Ah! | Ah! Sikuyaamini macho yangu. | mshangao |
Ala! | Ala! Umefika tayari! | mshangao |
Haha! | Haha! Umenivunja mbavu, bwana! | kicheko |
Ehee!, Enhe! | Enhe! Endelea, ninaipenda sana hadithi hiyo! | kuitikia |
Hmmm! | Hmmm! Chakula kitamu hicho! | kuitikia, kusifia |
Ebo! | Ebo! Tabia gani hiyo. | kukashifu, hasira |
Kefule! | Kefule! Umenifedhehesha sana. | hasira |
Wee! | Katamu alinegua kiuno na kucheza kwa madaha. Wee! Wavulana wakaduwaa. | kusifia |
La!, Hasha! | La! Sitaki kusikiliza upuuzi wako tena. | kukataa |
Hoyeee! | Wamama wote, hoyee! Hoyee! | kushangilia |
Huraa! | Huraa! Tumeshinda. | kushangilia |