Insha za Mada
Hizi ni insha ambazo mwaandishi hutakiwa kuzungumzia mada fulani kwa kutoa hoja ama maelezo. Insha hizi hazimhitaji mtahiniwa kuanza kusimulia hadithi yake bali ni kurejelea mada aliyopewa. Mwandishi wa insha kama hii anapaswa kuwa na hoja za kutosha kuhusu mada aliyopewa kabla ya kuanza kuiandika. Hoja zote zinapaswa kujitokeza katika masimulizi yenye mtiririko wala si kuorodhesha hoja, moja baada ya jingine.
Kwa mfano:
Andika insha juu ya:- Umuhimu wa kupanda miti
- Athari za kuavya mimba
- Namna ya kuboresha kilimo katika sehemu zenye ukame
- Mbinu za kukabiliana na wezi wa mifugo.
Insha hizi huwa insha halisia na hivyo mwaandishi hawezi kupigia chuku au kutoa hoja zisizo kweli. Kwa mara nyingi insha hizi hurejelea maswala ibuka katika jamii k.v njaa, ukimwi, kilimo, ufisadi, ukabila, n.k
Hata hivyo mwanafunzi anaweza kupata insha za mada zinazohitaji ubunifu, mapambo ya lugha n.k. Angalia mifano ifuatayo.
Andika insha juu ya:
- "Ndoto Niliyokuwa Nayo"
- "Siku Ambayo Sitaisahau Maishani"
- "Sherehe Niliyoihudhuria"
- "Ajali ya Barabarani Niliyoishuhudia"