Matumizi ya Viungo Mbalimbali
Katika mada hii, tunaangazia viambishimaneno ya silabi moja yanayotumika sana kwa Kiswahili kuwakilisha dhana mbalimbali.
Kwa sasa tumekuandalia matumizi ya:
Matumizi ya KI
Kiambishi Kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI
- Kiatu kilichochomeka kilikuwa kimeharibika.
- Kisiwa hiki kilichohamwa hakikaliki.
KI ya Masharti
- Ukitaka kufua dafu, lazima utie bidii.
- Ukicheka sana utavunjika mbavu.
- Nitazichukua zikianguka.
KI ya Mfanano - Kulinganisha(Vivumishi na vielezi vya Ki-Mfanano)
- Watu wa Mizukani wanaabudu kishetani.
- Amevalia mavazi ya kifalme.
- Msichana huyo huongea kimalaika.
KI ya Udogo
- Kijiji chao ni mahame.
- Kitabu kile kimejifunga.
Kuonyesha kinatendeka wakati mmoja na kitendo kingine
- Kesha alipobisha, Mganga Kuzimu alikuwa akila nzi.
- Tulimkuta akichoma mhindi. Mama alicheka mtoto akilia.
Kukanusha kauli ya kutendeka
- Wasichana warembo huoleka => Wasichana warembo hawaoleki.
- Sauti nzuri zinasikika => Sauti nzuri hazisikiki.
Kiambishi Kiwakilishi cha ngeli ya KI-VI
- Ikiona vyalea vyaundwa.
- Ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni.
Kutangulia majina ya lugha mbalimbali
- Ali Kiba huimba kwa Kiswahili.
- Kiingereza ndiyo lugha ya Wazungu kutoka Uingereza.
Matumizi ya KU
Kiambishi Kiwakilishi cha Ngeli ya mahali KU-KU
- Shuleni hakuna usalama.
- Huku kumekauka sana.
Kuanzisha vitenzi vya silabi moja au hali kamilifu ya kitendo.
- Ninataka kula.
- Walikuja jana asubuhi.
Kuanzisha nomino za kitenzi jina.
- Kuchekacheka kwake kulimsaliti.
- Kuimba kwenu hakunipendezi.
Kuanzisha vitenzi katika hali ya kawaida au kitenzi cha pili katika vitenzi sambamba.
- Kisu hutumika kukatia vitu.
- Wamekwenda kupiga ngoma.
Kiambishi cha Kukanusha Wakati Uliopita
- Maji yako hayakumwagika.
- Sikuingia kwenye chumba kile.
Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa/mtendewa nafsi ya pili.
- Watoto watakuchekelea ukivalia viatu vya manjano.
- Sijakueleza jinsi nilivyopambana na simba mwenye njaa.
Matumizi ya KWA
Kuonyesha umiliki wa mahali
- Sheila amekwenda kwa Bi Mashaka.
- Kwa akina Kawia ni mbali kutoka Vikwazoni.
Kutolea sababu au nia na Kuulizia Sababu
- Umeadhibiwa kwa kukosa nidhamu.
- Kali amelala mapema kwa kuwa anaenda shule mapema kesho.
- Ni kwa nini binadamu hawamheshimu Mungu
Kuonyesha sehemu ya kitu kizima (akisami)
- Katika mtihani walioufanya, Jabu alipata kumi na tatu kwa ishirini (13/20).
- Sehemu ya nne kwa tano (4/5) ya ndizi hizi imeoza.
Kulinganisha
- Timu yao ilishindwa mabao mawili kwa sufuri.
- Rita na Anita wanafanana kama shilingi kwa ya pili
Kuonyesha muda uliochukuliwa na kitendo
- Tulimsubiri kwa masaa mawili kisha tukaondoka.
- Yeye huoga kwa muda mfupi sana.
Kuelezea Ala au kitumizi
- Alikuwa akilima kwa jembe kuukuu.
- Walikuja kwa basi.
Kuelezea Mbinu, Jinsi au Namna
- Kaombi alipata pesa kwa kuandaa harambee.
- Mgonjwa aliongea kwa uchungu mwingi sana
Hutumika katika misemo
- Kesha na Nuru waliketi sako kwa bako.
- Mshindi alibebwa juu kwa juu
Matumizi ya NI
Kiambishi kiwakilishi cha Nafsi ya Kwanza umoja
- Nitakapokasirika watanitambua.
- Nitayainua macho yangu nitazame milima.
Kiunganishi cha wakati uliopo kuonyesha hali au sifa ya kitu.
- Katosha ni msichana mpole sana.
- Tegemeo letu ni kufika Mbinguni.
Kiambishi kiwakilishi cha kielezi cha mahali
- Nyuki wamefukuza wavulana uwanjani.
- Shimoni humu hamna nuru.
Kukanusha kauli ya kutendana, kutendeana
- Maji na mafuta hayatoshani uzani.
- Giza na nuru hazishirikiani.
Kiishio katika hali ya kuagiza, kuamuru au kuhimiza nafsi ya pili wingi
- Wahubirini watu wote.
- Ondokeni enyi msioijua njia.
- Pokeeni baraka tele.
Kukanusha kauli ya kutendeka
- Wasichana warembo huoleka => Wasichana warembo hawaoleki.
- Sauti nzuri zinasikika => Sauti nzuri hazisikiki.
Kiambishi kiwakilishi cha vivumishi viulizi nini na kwa nini
- Pilipili usiyoila ya kuwashiani?
- Mama amenipigia simu mara sita leo, sijui ananitakiani.
Matumizi ya KA
Kiambishi kiwakilishi cha Wakati Usiodhihirika
- Mama akamtuma mwanawe aende kuchota maji.
- Nikamwuliza anionyeshe sanduku lake.
Katika vitenzi sambamba - kitendo kimoja kinapofanyika baada ya kingine
- Alikula akashiba kisha akalala.
- Tulifika nyumbani, baba akatuuliza tumewaacha wapi fahali.
Kuagiza au Kuamuru
- 'Kalaleni!' Mama akawaamuru watoto.
- Kamwambie asirudi hapa tena.
Kiishio cha kauli ya kutendeka
- Kijana mtundu alipigwa akapigika.
- Tulijaribu kufungua mlango lakini haukufunguka.
Matumizi ya NA
Kiunganishi (cha Kujumuisha)
- Kikombe na bakuli ni vyombo vya jikoni.
- Jogoo alikatwa kichwa na kuchinjwa.
Kiambishi kiwakilishi cha wakati uliopo
- Ninapenda kusoma riwaya za Kiswahili.
- Ukuta unazidi kupasuka.
Kuonyesha umilikaji
- Selena ana sauti tamu.
- Kitanda kina kunguni weusi.
Kiishio cha kauli ya Kutendana na kutendeana
- Tuliwaona fahali wawili wakipigana.
- Mwalimu amepeana onyo la mwisho.
Matumizi ya PO
PO ya Mahali
- Mahali alipoanguka paliacha kuota nyasi.
- Hapo ndipo tulipoketi. Jumapili ifikapo tutakwenda Kisetoni.
PO ya Wakati
- Nilipomlilia aliisikia sauti ya dua langu.
- Kitumbua kilipikwa mayai yalipoletwa.
- Zitakaporudishwa tutazificha mbali.
PO ya Hisia(Hasira)
- Umenikosea sana! Po! Utakiona cha mtema kuni.