Sentensi za Kiswahili
Sentensi ni kundi la neno moja au maneno zaidi yenye kiima na kiarifa na inayofuata kanuni za sarufi.
Aina za Sentensi
1. Sentensi Sahili
Hizi ni sentensi zenye kishazi kimoja na huwakilisha wazo moja tu.
a) Sentensi sahili kutokana na kikundi tenzi pekee:
- Ninasoma => KT(T)
- Hajakuandikia barua => KT(T + N)
- Tulimwona nyoka mkubwa =>KT(T + N + V)
- Alikimbia haraka sana => KT(T + E + E)
b) Kikundi Nomino + Kikundi Tenzi
- Sakina anaimba. => KN(N) + KT(T)
- Latifa na Kanita wamejipamba vizuri. => KN(N + U + N) + KT(T + E)
- Jua kali liliwaka mchana kutwa. => KN(N + V) + KT(T + E + E)
- Runinga ya Bwana Kazito imeharibika tena. => KN (N + V + N + N) + KT (T + E)
2. Sentensi Ambatano.
Sentensi ambatano ni sentensi zenye zaidi ya kishazi huru kimoja na huwakilisha mawazo mawili au zaidi. Aghalabu sentensi hizi hutumia viunganishi(U) au alama za uakifishaji kama vile kituo(,) na nukta-nusu (;) ili kubainisha wazo moja toka nyingine.
a) Kuunganisha Sentensi Mbili:
- Chesi alisoma kwa bidii. Chesi alianguka mtihani.
=> Ingawa alisoma kwa bidii, Chesi alianguka mtihani. - Dadangu amerudi nyumbani. Dadangu amelala.
=>Dadangu amefika nyumbani na kulala.
Mifano mingine:
- Tulifika, tukaona, tukapiga na tukatawala.
- Leo inaonekana Karimi amejipamba akapambika.
3. Sentensi Changamano
Hizi ni sentensi zinazoundwa kwa kuunganisha kishazi huru pamoja na kishazi tegemezi au sentensi mbili kwa kutumia o-rejeshi ili kuleta zaidi ya wazo moja.
- Juma amenilitelea kitabu. Nilikuwa nimetafuta kitabu hicho kwa muda mrefu.
=> Juma ameniletea kitabu mbacho nilikuwa nimekitafuta kwa muda mrefu. - Yeye ni mwizi. Alipigwa jana jioni.
=> Yeye ndiye mwizi aliyepigwa jana jioni.
Mifano Zaidi:
- Nimemuona yule ninayemtafuta na neema zake.
- Ndoto zinazotisha ni za kishetani.
Tanbihi: Ili kutofautisha sentensi ambatano na changamano kwa urahisi, sentensi changamano hutumia o-rejeshi (k.m ambacho, ambaye, niliye- , nililo- n.k)