Sajili ya Matanga
Ni lugha inayotumiwa katika shughuli za mazishi au nyumbani kwa marehemu.
Sifa za Lugha ya Matanga/Mazishi
- Hutumia msamiati wa maneno ya huzuni kama vile waombolezaji, makiwa, kifo, mauti, pole n.k.
- Hutumia lugha ya kuliwaza/kufariji na kupa matumaini hasa kwa waombolezaji.
- Ni lugha yenye unyenyekevu isiyotumia maneno yanayokera.
- Hudhihirisha unyonge wa mwanadamu, kama asiye na mamlaka juu ya uhai wake.
- Huwa na mbinu rejeshi kurejelea maisha ya marehemu alipokuwa hai.
- Kwa mara nyingi hutumia maneno ya kusifu marehemu kutokana na aliyotenda.
- Wakati mwingine huwa ni lugha inayodhihiri hali ya kukata tamaa.
Mfano wa Sajili ya Matangani
"Waombolezaji wenzangu, kama mnavyojua tumekusanyika hapa kwa ajili ya kumsindikiza rafiki yetu amabye amelala hapa. Ikiwa kuna mtu alifikwa zaidi na msiba huu ni mimi. Marehemu alikuwa rafiki wangu wa dhati tuliyeshirikiana naye sana. Nilimjua marehemu tukifanya kazi katika soko la Mauzoduni na tangu siku hiyo tumeishi kama ndugu; kuomba radhi ukikosewa; kusaidiana, na kadhalika. "
Habari za kifo chake zilinipiga kwa mughdha. Sikuamini kwamba amekufa; kwamba sitamwona tena aushini mwangu. Ninasikitika sana lakini kwa kuwa Mungu hakosi, ninaamini kwamba alimpenda zaidi ya tulivyompenda. Ombi langu kwa Mungu ni moja, kwamba amweke rafiki yangu mahali pema peponi; au popote alipojitafutia siku zake za uhai; nami nitakapokufa anipeleke papo hapo tuendelee kuwa marafiki. Mwenzangu lala. Lala salama tutaonana siku moja"