Ushairi
Ushairi unaweza kuwa kipera cha fasihi simulizi (nyimbo) na pia katika fasihi andishi kwa sababu mashairi yanaweza kuwasilishwa kwa njia ya kukariri na pia kwa njia ya maandishi. Mashairi yanayoghanwa badala ya kuimbwa huitwa maghani.
Uchambuzi
Katika ushairi, tutaangalia:
- Aina za Mashairi - Kuainisha mashairi kulingana na idadi ya mishororo katika kila ubeti.
- Bahari za Ushairi - Muundo wa shairi kulingana vina, idadi ya mizani, vipande, mpangilio wa maneno n.k.
- Uchambuzi wa Mashairi - Mambo muhimu unayohitajika kuzingatia unapochambua shairi
- Uhuru wa Mshairi - Ukiukaji wa kanuni za sarufi
- Istilahi za Kishairi - Msamiati unaotumika katika ushairi km vina, mizani n.k
- Sifa za Ushairi - Sifa zinazobainisha ushairi kutokana na aina nyingine za sanaa.
- Umuhimu wa Ushairi - Umuhimu wa ushairi katika jamii.
Istilahi za Kishairi
Haya ni baadhi ya maneno ambayo hautakosa kukutana nayo unapozingatia ushairi. Ni muhimu mwanafunzi kuyajua vizuri.
- Shairi - ni sanaa ya maneno (utunzi maalum wa lugha ya kisanaa) unaotumia mpangilio na uteuzi maalum wa maneno na sauti ili kupitisha ujumbe fulani.
- Vina - ni silabi za mwisho katika kila kipande.
- Mizani - ni idadi ya silabi katika kila mshororo.
- Mshororo - ni msitari mmoja wa maneno katika shairi.
- Ubeti - ni kifungu cha mishororo kadhaa.
- Vipande - ni visehemu vya mshororo vilivyogawanywa kwa alama ya kituo(,)
- Ukwapi- kipande cha kwanza katika mshororo
- Mwandamo - Kipande cha tatu katika mshororo
- Ukingo - kipande cha nne katika mshororo
- Utao - kipande cha pili katika mshororo
- Mwanzo - mshororo wa kwanza katika ubeti
- Mloto - mshororo wa pili katika ubeti
- Kimalizio/Kiishio - mshororo wa mwisho katika ubeti usiorudiwarudiwa katika kila ubeti.
- Kibwagizo - mshororo wa mwisho katika ubeti unaorudiwarudiwa kila ubeti.
Sifa za Ushairi
- Huwa na vina, mizani, mishororo na beti
- Hutumia lugha teule
- Hufupisha au kurefusha maneno ili kutosheleza idadi ya mizani
- Mashairi hayazingatii kanuni za kisarufi. (Angalia uhuru wa mshairi)
- Hutumia mbinu za lugha
Umuhimu wa Mashairi
- Kuburudisha
- Kuhamasisha jamii
- Kukuza sanaa na ukwasi wa lugha
- Kuliwaza
- Kuelimisha
- Kuonya, kutahadharisha, kunasihi na kuelekeza
- Kupitisha ujumbe fulani
- Kusifia mtu au kitu
- Kukejeli au kukemea mambo yanayoenda kinyume na maadili ya jamii