Maghani Katika Fasihi Simulizi
Maghani ni tungo zinazotolewa kwa kughanwa (nusu kuimbwa nusu kukaririwa) Maghani yanaweza kuambatanishwa na ala za muziki au kughanwa kwa mdomo tu.
Aina za Maghani
Zipo fani mbali mbali za maghani ambazo zimeainishwa katika tanzu mbili kuu:
Maghani ya Masimulizi
Lengo la maghani ya aina hii ni kusimulia kisa fulani, historia, n.k.
Kuna fani mbili za Maghani ya Masimulizi:
a) Tendi
Tendi ni ushairi mrefu unaosimulia matukio ya kishujuaa. Tendi zinaposimuliwa huandamana na ala za muziki.
Sifa za Tendi:
- Ni ushairi mrefu
- Husimulia matendo ya kishujaa kwa njia kishairi
- Husimuliwa badala ya kuimbwa
- Huandamana na ala za muziki
- Husimulia visa vya kihistoria
- Hutungwa papo kwa hapo
b) Rara
Hizi ni hadithi fupi za kishairi zenye visa vya kusisimua, zinazosimuliwa zikiambatanishwa na ala za muziki. Aghalabu hughanwa na watoto; na hutumika kama michezo ya watoto.
Sifa za Rara
- Ni hadithi fupi za kishairi
- Husimulia visa vya kusisimua
- Zinaweza kuimbwa au kusimuliwa
- Huambatana na ala za muziki
- Aghalabu huwa ni visa vya kubuni
Maghani ya Kawaida (Sifo)
Maghani ya Kawaida ni maghani yanayosifia mtu, kitu au hali katika jamii
a) Majigambo au Kivugo
Haya ni maghani ambayo mtunzi hujisifia (kujigamba) namna alivyo hodari katika nyanja fulani. Tungo hizi hutumia chuku na maneno ya kejeli kuwadunisha wapinzani wa mtunzi.
Sifa za Majigambo
- Hutumia nafsi ya kwanza
- Msimulizi hutumia maneno ya kujigamba
- Msimulizi hutumia chuku kwa wingi ili kujisifu
- Hutungwa kwa ubunifu mkubwa na hutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara n.k
- Majigambo mengi huwa mafupi, lakini baadhi yake huwa marefu.
- Huwa na matendo matukufu ya msimulizi
- Huwa na ahadi za matendo kutoka kwa msimulizi
b) Tondozi
Tondozi ni aina ya sifo ambayo husifia watu mashuhuri katika jamii kama vile viongozi
Sifa za Tondozi
- Huwa ni ushairi wa kusimuliwa
- Husifia mtu mwengine, mtu mashuhuri
- Hutumia chuku
- Hutumia mbinu kama sitiari, vidokezi, ishara n.k
- Hutaja matendo makubwa ya kiongozi anayesifiwa
Pembezi
Pembezi ni maghani ya kumsifu mpenzi.
Sifa za Pembezi
- Humsifu mpenzi wa mtu
- Aghalabu huwa ushairi mfupi
- Hutumia tamathali za lugha kwa wingi kama vile ishara kusimulia umbo la mpenzi
- Pembezi zinaweza kuandamana na ngoma
ii) Pembezi - tungo za sifa. Zinaweza kusifia kundi fulani la watu, wanyama, njaa, mvua, n.k