Isimu Jamii
Isimu Jamii (social linguistics) - ni tawi la isimu (elimu ya lugha) linalochunguza namna lugha inavyotumika katika jamii na uhusiano baina yake. Tawi hili huzingatia matumizi ya lugha katika mazingira tofauti; aina mbali mbali za lugha na mazingira yake; uhusiano kati ya lugha na utamaduni wa jamii inayoitumia.
- Istilahi za Isimu Jamii
- Aina za Lugha
Istilahi za Isimu Jamii
- Isimu (linguistics) - ni mtalaa ambao huchunguza, huchanganua na pia kuchambua na kufafanua lugha kama mfumo wa mawasiliano baina ya wanadamu.
- Lugha - ni chombo cha mawasiliano baina ya watu. Lugha huzingatia mpangilio maalum wa sauti, maneno na sentensi.
- Sajili - ni mukhtadha/rejista mbalimbali au mitindo maalum ya lugha katika mazingira/hali mbalimbali. Mifano ya sajili ni kama vile lugha ya hospitalini, shuleni, sajili ya dini, biashara, kisiasa, michezo,
- Fonolojia - ni tawi la sayansi ya isimu linaloshughulikia uchunguzi wa mfumo wa sauti katika lugha fulani, kwa mfano ugawanyaji wa irabu na konsonanti. Fonolojia hutumika kuunda alfabeti katika lugha fulani. Aghalabu kila lugha hutumia mfumo fulani wa sauti mahususi katika lugha hiyo pekee.
- Fonetiki - huchunguza sauti zinazotamkwa na binadamu bila kuzingatia lugha yoyote.
- Mofolojia - (au sarufi maumbo) ni tawi la isimu linalochunguza maneno ya lugha fulani, aina za maneno katika lugha, hasa upangaji wa mofimu mbalimbali zitumikazo kwa ajili ya kuunda maneno hayo. Kwa mfano, lugha ya Kiswahili hutumia mbinu kadhaa kuunda maneno kulingana na mpangilio wa mofimu. Kwa mfano, neno 'lima' linaweza kutumika kuunda maneno mengine katika Kiswahili k.m mkulima, kilimo, nimelima, limika n.k Katika kubadilisha mofimu hizi, tunaweza kubadilisha neno moja kutoka aina moja(kitenzi) hadi nyingine (nomino) n.k
- Sintaksi - (au sarufi miundo) ni tawi la isimu au taaluma ya sarufi inayoshughulikia jinsi vikundi vya maneno na sentensi mbalimbali zinajengwa katika lugha. Sintaksia huangazia kanuni au sheria za lugha. Kila lugha huwa na sheria zake za kuambatanisha maneno kama vile jinsi ya kufuatanisha vitenzi, nomino na vielezi. Kwa mfano: Mtoto yako shiba ni sentensi isiyokuwa na sintaksi. Sentensi sawa ingekuwa: Mtoto wako ameshiba.
- Semantiki - ni tawi la isimu linalochunguza maana halisia (mantiki) ya maneno, kifungu au sentensi katika lugha. Sentensi isiyokuwa na mantiki ni sentensi inayotoa maana ambayo haiwezekani katika uhalisia. Sentensi inaweza kuwa sawa kisintaksia lakini iwe na makosa ya kimantiki. Kwa mfano: Kiatu cha mbwa kimefutwa kazi kwa sababu kumi ni kubwa kama hewa.
Aina za Lugha Katika Isimu Jamii
- Lafudhi - Ni upekee wa mtu katika matamshi (accent) unaoathiriwa na lugha ya mama, mazingira yake ya kijiografia au kiwango ujuzi wake wa lugha.
- Lahaja - ni vijilugha vinavyoibuka kwa lugha moja kuu kutokana na tofauti za kijiografia baina ya wazungumzaji wa lugha hiyo. Kwa mfano lugha ya Kiswahili ina lahaja kadhaa kama vile Kimtang'ata, Kilamu, Kimvita, n.k. Tofauti baina ya lufudhi ni kama msamiati, muundo wa sentensi au matamshi.
- Lugha rasmi - ni lugha inayotumika katika shughuli za kiofisi ama ya wakati wa mawasiliano rasmi katika taifa fulani. Kwa mfano, lugha rasmi nchini Kenya ni Kiingereza.
- Lugha rasimi - ni mtindo wa lugha uliotumiwa na mtu/watu fulani mashuhuri (zamani) na ambao huonekana kuwa mtindo bora wa lugha unaofaa kuigwa na wengine. Kwa mfano lugha ya Shakespeare.
- Lugha ya taifa - ni lugha inayoteuliwa na taifa fulani kama chombo cha mawasiliano baina ya wananchi, kwa maana inazungumzwa na wananchi wengi katika taifa hilo. Lugha ya taifa, nchini Kenya ni Kiswahili; Uganda ni Kiganda.
- Lugha Sanifu - Ni lugha iliyokarabatiwa na sheria zake (k.v muundo wa sentensi, msamiati, sarufi, n.k) kubainishwa na kuandikwa, na kwa hivyo huzingatia sarufi maalum na upatanisho sahihi wa sentensi. Kwa mfano: Kiswahili sanifu - ni lugha isiyokuwa na makosa ya kisarufi.
- Lingua Franka - Ni lugha inayoteuliwa miongoni watu wenye asili tofauti wasiozungumza lugha moja ili iwe lugha ya kuwaunganisha katika shughuli rasmi au za kibiashara.
- Pijini - ni lugha inayozaliwa kutokana na mchanganyo wa lugha zaidi ya moja. Kwa mfano. Sheng' (lugha ya vijana mitaani nchini ni lugha iliyoibuka kutoka kwa Kiswahili na Kiingereza.
- Krioli - Ni pijini iliyokomaa na kukubalika.
- Lugha mame - hii ni lugha isiyokua na ambayo hubaki kati umbo lake la awali. Kwa mfano lugha ya Kilatini haibadiliki na hivyo hutumika katika kubuni majina ya kisayansi, n.k.
- Lugha azali - ni lugha inayozaa lugha nyinginezo.
- Misimu - ni lugha yenye maneno ya kisiri ambayo hutumiwa na kikundi fulani cha watu katika jamii, inayoeleweka tu baina yao. Misimu huibuka na kutoweka baada ya muda.