Nyakati za Kiswahili

Nyakati katika lugha hutuonyesha kitendo chafanyika lini.

Mifano ya Nyakati

Wakati Uliopita - LI

Wakati huu hurejelea kitendo kilichofanyika muda mrefu uliopita. Vitenzi katika wakati uliopita hutumia kiambishi "LI"

kwa mfano : a-li-sema, ni-li-fika, wa-li-timuliwa

Wakati Timilifu - Uliopita Muda Mfupi - ME

Wakati timilifu huonyesha kitendo ambacho kimekamilika sasa hivi au muda usio mrefu. Hutumia kiambishi ME katika vitenzi.

kwa mfano: nimeshiba, limeanguka, kimeharibika

Wakati Uliopo - NA

Wakati uliopo huonyesha kitendo kinachoendela kufanyika sasa hivi. Hutumia kiambishi "NA" katika vitenzi.

kwa mfano: a-na-soma, tu-na-kueleza, zi-na-angamia

Wakati Ujao - TA

Huchukua kiambishi "TA" na hurejelea kitendo ambacho bado hakijafanyika lakini kinatarajiwa kufanyika..

kwa mfano: atakupa, kitajulikana, utapokelewa

Wakati wa Mazoea - HU

Hutumia kiambishi "HU" na hurejelea kitendo ambacho hufanyika mara kwa mara au kila siku n.k.

kwa mfano: hutembea, husoma, huzilinda

Wakati Usiodhihirika - A

Hutumia kiambishi cha ngeli au nafsi pamoja na kiungo "A" kurejelea kitendo kinachoendelea kutendeka katika wakati usiodhihirika.

kwa mfano: achukua, zapepea, twaangamia

Wakati Timilifu Usiodhihirika - KA

Hutumia kiungo "KA" kurejelea kitendo ambacho kinakamilika katika wakati usiojulika. Pia hutumika kurejelea kitendo kifanyika baada ya kingine. Hutumiwa katika masimulizi.

kwa mfano: ikawalemea, tukazichukua, likampendeza