Vitenzi (T)

Vitenzi ni maneno yanayosimamia kitendo. Kila kitenzi huwa na shina la kitenzi (sehemu ndogo zaidi ya kitenzi ambayo ndiyo huwakilisha tendo hilo). Shina la kitenzi huambatanishwa na viambishi ili kutoa maana iliyokusudiwa kama vile mtendaji, mtendewa, wakati kitendo kinafanyika na pia kauli ya kitenzi hicho.


Aina za Vitenzi


Vitenzi Halisi

Hivi ni vitenzi vinavyorejelea kitendo moja kwa moja. Vitenzi halisi vinapoambatanishwa na vitenzi vidogo katika sentensi, huitwa vitenzi vikuu.

k.m: soma, kula, sikiza
 • Waziri Mwasimba aliwasili jana kutoka ng'ambo.
 • Kawia atapikia wageni.
 • Funga mlango wa dirisha.

Vitenzi Visaidizi

Vitenzi visaidizi hutangulia vitenzi halisi (vitenzi vikuu) katika sentensi ili kuleta maana inayokusudiwa kulingana na wakati au hali.

k.m: -kuwa, -ngali,
 • Jua lilikuwa limewaka sana.
 • Bi Safina angali analala

Vitenzi Vishirikishi

Vitenzi vishirikishi hutumika kuelezea hali iliyopo au mazingira. Kuna aina mbili za vitenzi vishirikishi:

a) Vitenzi Vishirikishi Vipungufu - havichukua viambishi vyovyote.

k.m: ni, si, yu
 • Kaka yako ni mjanja sana.
 • Huyo si mtoto wangu!
 • Paka wake yu hapa.

b) Vitenzi Vishirikishi Vikamilifu - huchukua viambishi vya nafsi au ngeli. Vitenzi hivi vinaweza kusimama peke yake au vinaweza kufuatiliwa na vitenzi vikuu.

k.m: ndiye, ndio, ndipo
 • Sanita ndiye mkurugenzi wa kampuni
 • Huku ndiko kulikoibiwa

Muundo wa Vitenzi

Kwa kuzingatia muundo wa vitenzi, tunaweza kuweka vitenzi katika aina zifuatazo:

 1. Vitenzi vya Silabi Moja
 2. Vitenzi vya Kigeni
 3. Vitenzi vya Kibantu

Vitenzi vya Silabi Moja

Hivi ni vitenzi vyenye silabi moja pekee. Ili kuleta maana kamili, vitenzi hivi huambatanishwa na kiungo KU- katika kauli ya kutenda. Kama vitenzi vingine, vitenzi vya silabi moja vinaweza kunyambuliwa.

k.m: soma, kula, sikiza
 1. -cha - kucha - jua linapochomoza asubuhi k.m kumekucha
 2. -fa - kufa - kuacha kupumua, kupoteza uhai k.m amekufa
 3. -ja- kuja - fika mahali hapa k.m nimekuja
 4. -la- kula - kutia chakula mdomoni k.m anakula
 5. -nya- kunya - kutoa mabaki ya chakula toka tumboni k.m mtoto amekunya
 6. -nywa- kunywa - kutia kinywaji kama vile maji au maziwa mdomoni k.m ninakunywa uji
 7. -pa- kupa - kumkabithi/kumpatia mtu kitu k.m amenipa pesa
 8. -pwa- kupwa - kujaa hadi pomoni - k.m kisima kimekupwa maji
 9. -twa- kutwa - jua linapozama magharibi na usiku kuingia k.m kumekutwa
 10. -wa- kuwa - kutokea katika hali au mahali fulani k.m alikuwa

Vitenzi vya Kigeni

Hivi ni vitenzi vyenye asili kutoka kwa lugha nyingine badala ya Kibantu. Baadhi ya lugha hizo ni Kiarabu, Kizungu, Kireno, Kihispania n.k. Vitenzi hivi havifuatilii muundo wa kawaida wa vitenzi vya Kiswahili ambavyo huishia kwa sauti -a. Badala yake, vitenzi hivi huishia kwa sauti nyingine kama vile -e, i, -o, na u

k.m: haribu, tubu, shukuru, salimu, thamini, amini, samehe, baleghe

Vitenzi vya Kibantu

Hivi ni vitenzi vyenye asili ya Kibantu na ambavyo huishia kwa sauti -a. Kitengo hiki hujumuisha asilimia kubwa zaidi ya vitenzi vya Kiswahili

k.m: simama, shika, tembea, beba, soma, lia