Ngeli za Kiswahili
Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Katika mfumo wa kisasa (na unaokubalika), ngeli huundwa kwa kuunganisha viambishi viwakilishi vya nomino.
Kwa mfano, neno kitabu. Tunasema, "Kitabu kimepotea - Vitabu vimepotea."
Kwa kuunganisha kiambishi "KI"(umoja) na VI(wingi), tunapata ngeli ya KI-VI. Ni muhimu kusisitiza kwamba tunazingatia viambishi, wala si silabi ya kwanza.
Hivyo basi, maneno yasioyoanza kwa KI-VI kama vile chama -vyama yatakuwa katika ngeli ya KI-VI kwa kuwa yanachukua kiambishi KI => (Chama kimevunjwa - Vyama vimevunjwa.) Vivyo hivyo, kunayo majina yanayoanza kwa KI-VI yasiyokuwa katika ngeli ya KI-VI maadam yanachukua viambishi tofauti. k.v: kijana => A-WA (kijana amefika- vijana wamefika).
Tumekuandalia majedwali matatu kukupa mukhtasari wa ngeli zote za Kiswahili na jinsi baadhi ya maneno/viambishi vinavyobadilika kutoka ngeli moja hadi nyingine.
a) Jedwali la kwanza linakupatia ngeli, maelezo yake, na mifano ya majina:
NGELI | MAELEZO | MIFANO |
A-WA | Hii ni ngeli ya majina ya viumbe wenye uhai k.v watu, wanyama, ndege, wadudu, miungu, malaika n.k Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwa sauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi. Hata hivyo baadhi ya majina huchukua miundo tofauti. | mtu - watu |
KI-VI | Ni ngeli ya majina ya vitu visivyo hai, yanayoanza kwa KI- au CH- (umoja); na VI- au VY- (wingi). Pia ngeli hii hujumuisha majina ya vitu vingine katika hali ya udogo. k.v kitoto. | kitu - vitu |
LI-YA | Hujumuisha majina ya vitu visivyo hai pamoja na yale ya ukubwa k.v jitu. Majina yake huchukua miundo mbalimbali. Baadhi yake huchukua muundo wa JI-MA (jicho-macho), lakini yanaweza kuanza kwa herufi yoyote. Kwa wingi, majina haya huanza kwa MA- au ME-. | jani - majani |
U-I | Huwakilisha majina ya vitu visivyo hai, yaanzayo kwa sauti M- (umoja) na MI(wingi). | mti - miti |
U-ZI | Hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI- kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi. Majina yenye silabi tatu au zaidi hubadilishwa kwa wingi kwa kutoa sauti /u/' k.v ukuta-kuta. Majina ya silabi mbili huongezewa /ny/ katika wingi. k.v ufa - nyufa | ukuta - kuta |
I-ZI | Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). Mengi yake huanza kwa sauti /u/, /ng/, /ny/, /mb/, n.k | nyumba - nyumba |
U-YA | Ni majina machache mno yanayochukua kiambishi U(umoja) na YA(wingi). | uyoga - mayoga |
YA-YA | Hii ni ngeli ya vitu visivyoweza kuhesabika (nomino za wingi). Hayana umoja. Mengi ya majina haya huanza kwa MA- lakini yanaweza kuchukua muundo wowote. | maji |
I-I | Ni ngeli ya majina ya wingi ambayo huchukua kiambishi I- kwa umoja na pia kwa wingi. Majina haya hayana muundo maalum. | sukari |
U-U | Majina ya nomino za wingi yanayoanza kwa sauti /u/ au /m/. Hayana wingi. | unga |
PA-PA | Ni ngeli ya mahali/pahali - maalum. | mahali |
KU-KU | Ngeli ya mahali - kwa ujumla. Aidha, hujumuisha nomino za kitenzi-jina | uwanjani |
MU-MU | Ngeli ya mahali - ndani. | shimoni |
b) Jedwali la pili linaangazia jinsi ngeli mbalimbali zinavyotumia "a-nganifu", viashiria na viashiria visisitizi.
NGELI | A- UNGANIFU | VIASHIRIA | VIASHIRIA VISISITIZI | ||||
KARIBU | MBALI KIDOGO | MBALI | KARIBU | MBALI KIDOGO | MBALI | ||
A-WA | wa wa | huyu hawa | huyo hao | yule wale | yuyu huyu wawa hawa | yuyo huyo ao hao | yule yule wale wale |
KI-VI | cha vya | hiki hivi | hicho hivyo | kile vile | kiki hiki vivi hivi | kicho hicho vivyo hivyo | kile kile vile vile |
LI-YA | la ya | hili haya | hilo hayo | lile yale | lili hili yaya haya | lilo hilo yayo hayo | lile lile yale yale |
U-I | wa ya | huu hii | huo hiyo | ule ile | uu huu ii hii | uo huo iyo hiyo | ule ule ile ile |
U-ZI | wa za | huu hizi | huo hizo | ule zile | uu huu zizi hizi | uo huo zizo hizo | ule ule zile zile |
I-ZI | ya za | hii hizi | hiyo hizo | ile zile | ii hii zizi hizi | iyo hiyo zizo hizo | ile ile zile zile |
U-YA | wa ya | huu haya | huo hayo | ule yale | uu huu yaya haya | uo huo yayo hayo | ule ule yale yale |
YA-YA | ya | haya | hayo | yale | yaya haya | yayo hayo | yale yale |
I-I | ya | hii | hiyo | ile | ii hii | iyo hiyo | ile ile |
U-U | wa | huu | huo | ule | uu huu | uo huo | ule ule |
PA-PA | pa | hapa | hapo | pale | papa hapa | papo hapo | pale pale |
KU-KU | kwa | huku | huko | kule | kuku huku | kuko huko | kule kule |
MU-MU | mwa | humu | humo | mle | mumu humu | mumo humo | mle mle |
c) Jedwali la pili linaangazia virejeshi(-o, amba-, -enye, -enyewe), ote, o-ote, ingi, ingine n.k kulingana na ngeli mbalimbali.
NGELI | KIREJESHI | O-REJESHI (AMBA-) | ENYE | ENYEWE | OTE | O-OTE | INGI | INGINE |
A-WA | ye o | ambaye ambao | mwenye wenye | mwenyewe wenyewe | wote wote | yeyote wowote | mwingi wengi | mwengine wengine |
KI-VI | cho vyo | ambacho ambavyo | chenye vyenye | chenyewe vyenyewe | chote vyote | chochote vyovyote | kingi vingi | kingine vingine |
LI-YA | lo yo | ambalo ambayo | lenye yenye | lenyewe yenyewe | lote yote | lolote yoyote | jingi mengi | jingine mengine |
U-I | o yo | ambao ambayo | wenye yenye | wenyewe yenyewe | wote yote | wowote yoyote | mwingi mingi | mwingine mingine |
U-ZI | o zo | ambao ambazo | wenye zenye | wenyewe zenyewe | wote zote | wowote zozote | mwingi nyingi | mwingine nyingine |
I-ZI | yo zo | ambayo ambazo | yenye zenye | yenyewe zenyewe | yote zote | yoyote zozote | nyingi nyingi | nyingine nyingine |
U-YA | o yo | ambao ambayo | wenye yenye | wenyewe yenyewe | wote yote | wowote yoyote | mwingi mengi | mwingine mengine |
YA-YA | yo | ambayo | yenye | yenyewe | yote | yoyote | mengi | mengine |
I-I | yo | ambayo | yenye | yenyewe | yote | yoyote | nyingi | nyingine |
U-U | o | ambao | wenye | wenyewe | wote | wowote | mwingi | mwingine |
PA-PA | po | ambapo | penye | penyewe | pote | popote | pengine | |
KU-KU | ko | ambako | kwenye | kwenyewe | kote | kokote | kwingi | kwengine |
MU-MU | mo | ambamo | mwenye | mwenyewe | mote | momote | mengine |