Fasihi Simulizi

Fasihi Simulizi ni utanzu wa fasihi ambao unawakilisha sanaa ya lugha inayopitishwa kutoka kwa kizazi hadi kizazi kwa njia ya maneno/masimulizi ya mdomo.

Sifa za Fasihi Simulizi

 1. Hupitishwa kwa njia ya mdomo
 2. Ufanisi wa sanaa katika fasihi simulizi hutegemea uwezo wa msimulizi, au wahusika
 3. Masimulizi yake yanaweza kuathiriwa na mazingira, hisia na hali
 4. Ni mali ya jamii. Hakuna mtu fulani anayemiliki sanaa katika fasihi simulizi.
 5. Inaweza kubadilika kutoka kizazi hadi kizazi, au mazingira mbalimbali kwa sababu hutegemea kumbukumbu ya msimulizi.
 6. Aghalabu huwa na funzo fulani

Umuhimu wa Fasihi Simulizi

 1. Kuburudisha - Hufurahisha na kuchangamsha hadhira
 2. Kunasihi- kutolea mawaidha na kuonyesha mwelekeo unaotarajiwa katika jamii
 3. Kuelimisha watu kuhusu vitu mbalimbali hasa mazingira yao
 4. Kutambulisha jamii - jamii mbalimbali husifika kutokana na sanaa zao katika fasihi simulizi kama vile nyimbo
 5. Kuhifadhi na kudumisha utamaduni wa jamii
 6. Kuunganisha watu - huleta watu pamoja
 7. Kukuza lugha - fasihi huimarisha lugha kwa kuwa hutumia mbinu mbalimbali za lugha.
 8. Kuliwaza - hutoa huzuni na kuleta matumaini.
 9. Kupitisha muda - wakati mwingine fasihi simulizi hutumika kupitisha muda.