Shadda na Kiimbo
Shada(Shadda) na Kiimbo ni namna ya kutamka neno au fungu la maneno kwa namna tofauti kuleta maana mbalimbali.
Shadda / Shada - (Stress)
Shadda ni mkazo wa silabi. Maneno ya Kiswahili huwa na silabi moja ambayo hutamkwa kwa nguvu zaidi kuliko silabi nyingine. Unapotamka silabi iliyotiwa mkazo (shada), sauti hupandishwa juu kiasi.
Maneno mengi ya Kiswahili, hasa yale yenye asili ya Kibantu hutia mkazo katika silabi ya pili kutoka mwisho.
Kwa mfano:ma'ma, sandu'ku, kita'bu, tulikoto'ka, buruda'ni, baraba'ra (njia)
Baadhi ya maneno yenye asili ya kigeni, huwa na shada katika silabi nyingine.
Kwa mfano:bara'bara (sawa sawa), mukhta'sari,
Kiimbo - (Intonation)
Kiimbo ni sauti maalum inayojitokeza unapotamka maneno fulani. Kiimbo husaidia kuleta maana kamili ya sentensi iliyokusudiwa. Kwa kutamka sentensi kwa sauti fulani 'ya kiwimbo', tunaweza kubainisha kauli ya kawaida, swali, hisia n.k.
Sentensi au maneno yanapotamkwa kwa viimbo mbalimbali, hutoa dhana tofauti. Katika uandishi, Viimbo husaidiwa na alama za uakifishaji ili kumwelekeza msomaji asome kwa kiimbo kilichokusudiwa.
a) Kuulizia Swali (?)
Tunainua sauti tunapouliza swali ili kulitofautisha na sentensi ya kawaida.
k.m Ulisoma kitabu nilichokupatia?
b) Kuonyesha Hisia (!)
Tunapotoa hisia, aghalabu kiimbo huenda juu.
k.m Ajabu!
c) Kutoa Kauli (.)
Tunapotoa kauli (sentensi ya kawaida), aghalabu sauti huenda chini katika neno au silabi ya mwisho. Hata hivyo, sauti inaweza kubadilika kulingana na neno linalotiliwa mkazo katika sentensi.