Vielezi (E)
Vielezi ni maneno yanayotoa habari zaidi kuhusu kitendo kilivyofanyika. Pia vielezi hutoa habari zaidi kuhusu hali, vivumishi au vielezi vingine.
Aina za Vielezi
Vielezi vya Mahali
Vielezi vya mahali hutoa habari kuhusu mahali ambapo kitendo kilifanyika. Aghalabu vielezi hivi huundwa kwa kutumia jina la mahali au kwa kuongeza kiungo -NI mwishoni mwa neno linaloashiria mahali.
- Mtoto huyo hajatulia nyumbani tangu alipotoka Mombasa.
- Msipitie sokoni mkienda kanisani.
Vielezi vya Wakati
Huelezea zaidi kuhusu wakati kitendo kipofanyika
- Mzee Kasorogani amesema kwamba ataoga mwaka ujao
- Musa alilazimishwa kuchimba mtaro saa sita usiku
- Kisaka na Musa watakutana kesho
Vielezi vya Idadi
Vielezi vya idadi hutulezea kitendo kilifanyika mara ngapi
a) Idadi Kamili
Vielezi vya Idadi Kamili hutaja idadi kamili ya mara ngapi kitendo kilifanyika.
- Gibi alimzaba kofi mara tatu na kisha akakimbia.
- Daktari alimwagiza mama huyo achukue dawa mara tatu kwa siku na arudi hospitalini siku mbili kwa mwezi
b) Idadi Isiyodhihirika
Vielezi vya Idadi Isiyodhirika huelezea kiasi ambacho kitendo kilifanyika bila kutaja kiasi kamili
- Mwizi wa kuku alipigwa mara kadhaa kabla ya kuokolewa na polisi.
- Yeye hunipigia simu mara kwa mara
VIelezi Vya Namna
Huelezea jinsi au namna kitendo kinavyofanyika. Kitendo kinaweza kufanyika kwa namna mbalimbali. Hivyo basi kuna aina mbalimbali za vielezi vya namna:
a) Vielezi vya Namna Halisi
Hutufahamisha jinsi kitendo kinavyofanyika kwa kutumia maneno halisi (bila kuambatanishwa na maneno mengine au viambishi vingine).
- Kioo cha bibi harusi kilianguka na kuharibika vibaya
- Mama alipika chakula upesi
- Amepigwa kalamu kwa kufanya kazi kiholela
b) Vielezi vya Namna Hali
Hutufahamisha hali ambayo kitendo kilifanyika. Vielezi hivi hujihusisha na tabia ya kitu/mtendaji wa kitendo
- Bibi harusi aliingia kanisani kwa madaha
- Mtoto alilia kwa maumivu mengi
c) Vielezi vya Namna Kitumizi/Ala
Hutoa habari kuhusu kifaa, ala au mbinu iliyotumiwa kufanya kitendo fulani
- Mkulima aliangusha mti mkubwa kwa shoka
- Mzee huyo alimpiga mke wake kwa bakora kabla ya kuchoma nguo zake kwa makaa
d) Vielezi Vikariri
Husisitiza kitendo kinavyofanyika kwa kutaja kielezi kinachorejelewa mara mbili mfululizo.
- Polisi walipoingia, wezi walitawanyika haraka haraka.
- Wanafunzi wengi hufanya kazi yao ovyo ovyo
e) Vielezi vya Ki-Mfanano
Vielezi mfanano hutumia KI-mfanano kuelezea kitendo kinavyofanyika kwa kulinganisha.
- Babake huongea kiungwana.
- Harida hutembea kijeshi
f) Vielezi Viigizi
Vielezi hivi huigiza sauti au mlio wa kitu, kitendo kitendo kilipofanyika kwa kutumia tanakali za sauti
- Mwanafunzi alitulia tuli mwalimu alipomzaba kofi pa!
- Kaswimu aliangusha simu changaraweni tifu na kujitumbukiza majini chubwi
g) Vielezi vya Vielezi
Vielezi hivi hutumika kuelezea kielezi kingine. Hivyo basi, hutanguliwa na kielezi badala ya kitendo
- Mamake Kajino alitembea polepole sana.
- Chungu kilivunjika vibaya kabisa
h) Vielezi vya Vivumishi
Hutoa habari zaidi kuhusu kivumishi
- Yeye ni mrefu sana
- Mtoto wake ana tabia nzuri mno