Methali ni tungo fupi za kisanaa ambazo hutoa wosia/nasaha kwa lugha ya mafumbo.
Sifa za Methali
-
Huwa na maana ya ndani na ya nje.
Maana ya ndani huwa fiche na huhitaji hekima kuitambua.
Maana ya juu huwa wazi kwani hurejelea vitu vinavyojulikana vizuri.
- Dua la kuku halimpati mwewe =>
- maana ya juu i wazi kwamba kilio na laana za kuku haziwezi kumwathiri mwewe alimnyang'anya kifaranga.
- Maana ya ndani ni kwamba kilio cha mnyonge asiye na uwezo hakiwezi kumhangaisha mwenye nguvu/ mtesi wake.
-
Methali huwa na vipande viwili
- Mtaka cha mvunguni, sharti ainame
- Mpanda ngazi, hushuka
- Hasira, hasaraMifano ya Methali
-
Baadhi ya methali hutumia mbinu za lugha
- Takriri => kinga na kinga ndipo moto huwakapo
- Istiara => mzigo wa mwenzio ni kanda la usufi
- Tashbihi => mapenzi ni kama kikohozi, hayafichiki
- Kejeli => Ganda la muwa la jana chungu kaona kivuno
- Chuku => maji ya kifuu bahari ya chungu
- Tashihisi => sikio la kufa halisikii dawa
-
Methali huwa na mazingira
- Ukulima => mchagua jembe si mkulima
- Uvuvi => hasira za mkizi, furaha ya mvuvi
- Elimu => elimu ni mwangaza gizani hung'aa
- Familia => Uchungu wa mwana aujuaye ni mzazi
-
Baadhi ya methali ni refu, nyingine ni fupi
- Cha mkufuu mwanafuu ha na akila hu, cha mwanafuu mkufuu hu na akila ha. (refu)
- Akiba haiozi (fupi)
-
Methali huwa na wakati - kuna methali za kale na za kisasa
- Mti mkuu ukigwa wana wa nyuni huyumba (kale)
- Mti mkuu ukianguka ndege huwa mashakani (kisasa)
-
Methali huwa na funzo
Hakuna methali isiyokuwa na funzo lake.
-
Baadhi ya Methali huwa na Ukinzani - kuwepo kwa methali nyingine inayopinga maana ya hiyo
- Ngoja ngoja huumiza matumbo; mstahimilifu hula mbivu
- fuata nyuki ufe mzingani; fuata nyuki ule asali
- mavi ya kale hayanuki; mavi ya kale hayaachi kunuka
-
Baadhi ya Methali huwa na maana sawa
- Haraka haraka haina baraka;
Polepole ndio mwendo;
Simba mwenda pole ndiye mla nyama
- Mchagua jembe si mkulima;
Mshoni hachagui nguo
Umuhimu wa Methali
- Methali huonya/hutahadharisha watu katika jamii dhidi ya maovu. k.v. Usipoziba ufa utajenga ukuta
- Methali hutoa mafunzo k.v bahari haivukwi kwa kuogelea
- Methali hutumiwa na waandishi, wazungumzaji na katika kazi mbali mbali za sanaa kama mapambo ya lugha
- Hutumika kutoa mawaidha katika jamii - mfano: asiyefunzwa na mama hufunzwa na ulimwengu
- Hutumika kuunganisha jamii pamoja. Kuna methali nyingi zinazosisitiza umoja k.m Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu; kidole kimoja hakivunji chawa.